Moja kati ya maswali ambayo watu wengi wangependa kuyapatia majibu kutoka kwa pande mbili, ni hali ya urafiki uliogeuka kuwa uhasimu wa kisiasa kati ya Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, swali ambalo limekutana na Lowassa.

Lowassa aliyekuwa kiongozi mkuu wa harakati za kumpigia kampeni rafiki yake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na baadae rafiki yake kumpa nafasi ya Uwaziri Mkuu aliyoimudu kabla ya kulazimika kujiudhuru mwaka 2008 kwa kashfa ya Richmond. Alikutana na upinzani mkubwa wa rafiki yake alipoamua kuwania urais mwaka 2015 akiwa ndani ya CCM na zaidi baada ya kuhamia Chadema.

Awali, wawili hao walieleza kuwa urafiki wao sio wa kukutana barabarani hivyo sio rahisi kuvurugika, lakini wengi wengependa kufahamu kuhusu hali ilivyo hivi sasa baada ya kupitia yaliyopita.

Hata hivyo, swali la Mwandishi wa Mwananchi aliyekutana na Lowassa uso kwa uso, ingawa lilionekana kuwa zuri mbele ya mwanasiasa huyo aliliweka kando.

Mwandishi: Mara kadhaa umekuwa ukisema urafiki wako na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete sio wa kuokota barabarani. Je, bado unaamini hivyo?

Lowassa: Hilo ni swali zuri, uliza jingine.

Jina la Lowassa ni miongoni mwa majina ‘yaliyokatwa’ na Kamati Kuu ya CCM chini ya Uenyekiti wa Dk. Kikwete baada ya kuwasilishwa kwa nia ya kupitisha majina matano kwa ajili ya kuwania nafasi ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Baada ya kukatwa, Lowassa alitokea upande wa pili akijiunga na Chadema iliyompa nafasi ya kugombea urais akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa.

Mwanasiasa huyo mkongwe alishika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu uliomalizika kwa kumpa ushindi Rais John Magufuli (CCM).

Ronaldo avishwa taji la ‘mfalme’ wa mitandao ya kijamii 2016
Polepole atangaza moto wa 'mageuzi ya makusudi' CCM