Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mizengo Pinda amepongeza uanzishwaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini hususani uanzishwaji wa mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge ikiwamo uchimbaji wa bwawa kubwa la umeme lililodaiwa litasababisha uharibifu wa mazingira.

Ameyasema shambani kwake eneo la Zinje nje kidogo ya jiji la Dodoma katika uzinduzi wa mradi wa kisasa wa bwawa la ufugaji samaki kupitia Pinda Farm, mradi uliozinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Mzee Mkongea Ally.

Amesema kuwa serikali ya Awamu ya Tano imekuwa jasiri bila kuhofia kitu chochote ikiwemo kuanzisha miradi mbalimbali katika nyanja za Elimu, Afya, Maji na Umeme Vijijini ambayo imeleta chachu kubwa ya maendeleo ya wananchi katika maeneo yao

”Huyu ndugu yetu ameonyesha jeuri isiyo ya kawaida, isiyo ya kawaida, kwanza katika mapambano ya rushwa, wazembe, wabadhirifu, wavivu, ameingia kwa gia ambayo imemshtua kila mmoja anasema usipofanya vizuri ni shida,”amesema Pinda

Aidha, amesema kuwa Rais Magufuli ameweza kurejesha nidhamu serikalini na kuweza kuongeza uwajibikaji kwa kila mmoja katika idara yake anayofanyiakazi.

Kwa upande wake Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde amesema kuwa mradi huo utakuwa chahu ya kuongeza ajira kwa vijana na watu mbalimbali, kwani mradi huo utahitaji wasimamizi ili uweze kufanya vizuri.

Naye msimamizi wa mradi huo, Bi. Tunu Pinda amesema kuwa mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 29.5 kwa kuweza kujenga mabwawa saba ya kufugia samaki.

Kesi ya Lissu kaa la moto, Mashinji anena ya Moyoni
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 16, 2019