Kocha Mkuu wa AS Vita Club Florent Ibenge amesema yupo tayari kupokea matokeo yoyote kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi dhidi ya Simba SC, utakaochezwa kesho Jumamosi (April 03) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.00 jioni.

Ibenge ametoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari leo mchana jijini Dar es salaam, ambapo amesema hawako tayari kujiweka kwenye presha kubwa katika mchezo huo, na aina yoyote ya matokeo yatakayopatikana watayapokea.

Ibenge amesema amefanya maandalizi ya kutosha na wachezaji wake wapo tayari kupambana na wenyeji Simba SC, ambao ana uhakika watawapa upinzani wa kutosha ndani ya dakika 90.

“Siku zote tumekuwa tukifurahia kucheza na ni furaha kubwa zaidi kucheza na timu kama Simba ambayo ni miongoni mwa timu bora na nzuri Afrika.”

“Tulicheza mchezo wa kwanza kule DR Congo na tukashindwa kufanya kama tulivyotarajia tukapoteza mchezo hivyo tumekuja hapa tukiamini tukicheza kama tulivyopanga tutapata matokeo tunayoyahitaji.”

“Tunafahamu tunahitajika kupata ushindi ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kufuzu lakini mwisho wa siku huu ni mpira wa miguu na tuko tayari kupokea matokeo yoyote iwe tutashinda, kutoka sare au kufungwa,” amesema Ibenge.

Naye mlinda mlango wa AS Vita Club Nathan Mabrouk amesema wanafahamu ugumu wa kucheza na Simba SC lakini wako tayari kukabiliana nao kwa dakka zote 90.

“Wachezaji wote tuko tayari na akili yetu tumeilekeza kwenye mchezo huu ambao tunahitajika kupata ushindi,” amesema Mabrouk.

AS Vita Club yenye alama nne, inahitaji matokeo ya ushindi tu katika mchezo wa kesho dhidi ya Simba ili iweke hai matumaini yake ya kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Barani Afrika msimu huu 2020/21.

Simba SC inaongoza msimamo wa Kundi A kwa kufikisha alama 10, ikifuatiwa na Al Ahly yenye alama 7, AS Vita inashika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 4 na AlMerrikh wanaburuza mkia kwa kupata alama moja kwenye michezo minne waliocheza.

Rashford amtaja Sadio Mane EPL
Matola: Matokea kesho lazima