Siku chache kabla ya kuanza kwa ‘Nginja Nginja’ za michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi, Kocha Mkuu wa AS Vita Club Florent Ibenge amefunguka kuhusu wapinzani wake kutoka Tanzania Simba SC.

AS Vita Club wataanzia nyumbani kwa kuikabili Simba SC Jumatano ya juma lijalo (Februari 12), mchezo ambao utatazamwa kama sehemu ya kuendeleza upinzani baina ya klabu hizo mbili, ambazo zilikutana mara mbili kwenye michuano hiyo msimu wa 2018/19.

Ibenge ameizungumzia Simba SC, baada ya kurejea mjini Kinshasa akitokea nchini Cameroon alipokua na timu ya taifa ya DR Congo kwenye Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’.

Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika amesema Simba SC imekua na maandalizi mazuri kabla ya kuikabili AS Vita Club, hivyo anatarajia upinzani mkubwa ambao utakua tofauti na ilivyokua misimu miwili iliyopita.

Amesema Simba SC wamepata wasaa kucheza michezo ya kirafiki kupitia michuano ya Simba Super Cup, kwa kucheza dhidi ya wapinzani wao wakubwa ndani ya DR Congo  (TP Mazembe) na Al Hilal ya Sudan, jambo ambalo anaamini limewajenga vyema kabla ya kukutana nao juma lijalo.

“Simba wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo dhidi yetu utakaochezwa juma lijalo hapa Kinshasa, kucheza dhidi ya Al Hilal na TP Mazembe kisha wakapata matokeo mzuri, ni wazi inaonesha wana kikosi imara na chenye malengo makubwa msimu huu, hivyo natarajia upinzani tofauti na ilivyokua misimu miwili iliyopita ambapo tuliwafunga 5-0 kabla ya sisi kupoteza Dar es salaam mabao 2-1.”

“Kwa upande wetu ushindi ni jambo la muhimu kwa kuwa tutakuwa nyumbani sehemu ambayo ni muhimu kwetu kuibuka na ushindi utakaotupa alama tatu muhimu, najua haitakuwa rahisi kwa kuwa ukiitazama Simba utaona kuwa ni timu nzuri lakini tutafanya kila liwezekanalo kuibuka na matokeo mazuri.” Amesema Ibenge.

AS Vita Club na Simba SC katika ligi ya mabingwa zote zipo kundi A sambamba na mabingwa watetezi Al Ahly pamoja na Al Mereikh ya Sudan.

Wanaume wanaongoza kufa kwa UKIMWI
Amshambulia mama mjamzito kwa bakora