Imefahamika kuwa, kiungo mshambuliaji wa mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC Ibrahim Ajib, amerudishwa kambini kwa masharti maalum, baada ya kuonesha utovu wa nidhamu wakati timu ilipokua kwenye mchakato wa kuanza kambi juma lililopita.

Ajib alitimuliwa kambini na kocha mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck huku akiwa na mabegi yake mgongoni kwa kosa la kuchelewa kuripoti, lakini mwanzoni mwa juma hili aliruhusiwa kujiunga na wenzake kwenye mazoezi yanayoendelea katika uwanja wa Mo Simba Arena.

Masharti aliyopewa kiungo huyo ambaye aliwahi kutimkia Young Africans misimu miwiwli iliyopita, ni kujituma sana kimchezo na kujirekebisha kinidhamu huku faini ikimhusu pia.

Adhabu ya Ajib imemalizika kwa sharti la kulipa faini ya Shilingi 200,000 ambayo atakatwa katika mshahara wake mwisho wa mwezi Mei kama sehemu ya utaratibu wa nidhamu wa Simba.

Mwanzoni mwa juma hili Ajib alifika kambini, Mbweni na kuzungumza na Sven mazungumzo mafupi kisha aliruhusiwa kuwa sehemu ya wachezaji na maisha yakaendelea.

Katika mazoezi hayo ya Simba, juzi jioni Ajib alikua katika kikosi cha wachezaji wa Simba ambao walifanya mazoezi katika uwanja Mo Simba Arena.

Katika mazoezi hayo Ajib alikutana na cha moto baada ya mazoezi kuanza saa 11:00 jioni kwani alikimbizwa mbio za kuzunguka uwanja huku Sven akiwa anamsimamia.

Ajib akiwa anakimbia mbio za kasi na polepole akizunguka uwanja mzima, Sven alikuwa akimsimamia huku wachezaji wengine wote wakiwa katikati ya uwanja wakiwa wanafanya mazoezi ya kawaida.

Mazoezi hayo ya kawaida kwa wachezaji wengine yalikuwa yakisimamiwa na kocha wa viungo, Adel Zrane aliyekuwa sambamba na kocha msaidizi Selemani Matola.

Mchezaji huyo hakuwa anakimbia mwenyewe bali alikuwa na wachezaji wengine Rashid Juma na Francis Kahata ambaye naye alikuwa anafanya mazoezi ya kwanza ya uwanjani akiwa na kikosi hicho tangu aliporejea nchini.

Sven alionekana kumkadhania Ajib na kumkomalia kutaka akimbie kwa kasi kama vile ambavyo alikuwa anataka mwenyewe na muda wote macho yalikuwa kwake.

Luc Eymael kurejea Tanzania Juni 06/07
Simba SC yamkana Shonga