Katibu wa baraza la wazee wa mabingwa wa soka Tanzania bara Young Africans, Ibrahim Akilimali ameshangazwa na taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu mpango wake wa kuwania nafasi ya mwenyekiti wa klabu hiyo, baada ya kujiuzulu kwa Yusufu Manji.

Akilimali ameshangazwa na taarifa hizo baada ya kutafutwa na kuzungumza na Dar24 kuhusu fununu hizo ambazo jana zilichukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii.

Mzee huyo aliyekua mstari wa mbele kupinga mabadiliko ya Young Africans kukodishwa kwenye kampuni ya Yanga Yetu, amesema ni kweli alizungumzia suala ya kuwa tayari kuwania nafasi ya uenyekiti wa klabu, lakini alikua anatania baada ya kuulizwa na mtu wake wa karibu.

“Jambo hilo nimelizungumza kweli, lakini haikua katika mpango wa kumaanisha ninadhamira ya kuwania kiti hicho, naamini haiwezekani kwa mimi kuwania nafasi ya uenyekiti wa Young Africans kutokana na sifa za elimu zilizoainishwa kwenye katiba.

“Katiba inaagiza anaetaka kuwania kiti cha uenyekiti wa Young Africans ni lazima awe na elimu ya chuo kikuu, mimi elimu hiyo sina, sasa nitawezaje kuingia kwenye mchakato huo wakati natambua sina sifa za elimu.

“Na hili limewekwa makusudi kwa ajili ya kutuzuia watu kama sisi tusigombee, lakini ingekua tofauti na hapo ningekua tayari nimeshatangaza katika mkutano na waandishi wa habari kuwa, nitagombea uenyekiti.

Hata hivyo Akilimali amehoji uhalali wa kuwa na viongozi wenye elimu ya juu, kwa kusema mpaka sasa wameshindwa kuiwezesha Young Africans kufikia lengo la kujiendesha kibiashara.

Amesema ni aibu kubwa, kwa sababu wanachama huwaamini watu wanaowachagua kwa elimu zao, lakini cha kushangaza wanapokuwa madarakani hujisahau na kushindwa kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya Young Africans.

Alvaro Morata Anukia Old Trafford
Idadi ya vifo yaongezeka jengo lililoteketea kwa moto Uingereza