Washambuliaji Mauro Icardi na Paulo Dybala wanatarajiwa kuchezesha pamoja katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Colombia utakaochezwa siku ya Jumatano jijini New York, Marekani.

Mpango wa wawili hao kuchezeshwa kwa pamoja, umekuja baada ya Mauro Icardi kujiunga na wenzake katika mazoezi ya pamoja kufuatia kupona majeraha ya misuli ya paja, huku Paulo Dybala akimaliza matatizo yake binafsi (matatizo ya kifamilia) na kurejea kambini rasmi.

Kocha wa muda wa kikosi cha Argentina Lionel Scaloni anatarajiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wanane, tofauti na alivyokipanga kikosi chake wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Guatemala waliokubali kibano cha mabao matatu kwa sifuri, juma lililopita.

Katika mchezo huo, mshambuliaji wa klabu ya  Fiorentina Giovanni Simeone alifunga bao la kwanza baada ya kuanza kuitumikia timu ya taifa ya wakubwa.

Katika mchezo huo, Scolani alitumia mfumo wa 4-3-3, lakini mpambano dhidi ya Colombia anatarajia kutumia mfumo wa 4-2-3-1.

Icardi ambaye mpaka sasa ameshaitumikia timu ya taifa katika michezo minne amekua na shauku ya kutaka kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha Argentina, baada ya kuachwa na kocha Jorge Sampaoli kabla ya fainali za kombe la dunia zilizounguruma nchini Urusi.

Alicheza michezo miwili ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018 dhidi ya Uruguay na Venezuela mwezi Septemba 2017, na bado hajaifungia Argentina bao.

Kikosi cha Argentina dhidi ya Colombia kinatarajiwa kuwa hivi: Armani; Bustos, Pezzella, Funes Mori, Acuna; Battaglia, Paredes; Meza, Dybala, Cervi na Icardi.

Mchungaji anusurika kifo, adaiwa kutumia nguvu za giza
Eti mtu anaogopa kuongea Kiswahili, haya ni maajabu kweli- JPM