Baada ya kikosi cha England kushindwa kutamba mbele ya Iceland usiku wa kuamkia hii leo, katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Euro 2016 kwa kukubali kufungwa mabao mawili kwa moja, kocha Roy Hodgson ametangaza kujiuzulu.

Hodgson mwenye umri wa miaka 68, alifikia maamuzi hayo kwa kuomba radhi, kwa kile kilichotokea uwanjani hapo jana ambapo ilionekana dhahir Iceland waliizidi mbinu timu yake.

Babu huyo alisema ni vigumu kuchukua maamuzi magumu kama hayo ya kujiuzulu, lakini hana budi kufanya hivyo kutokana na kutimiza suala la uwajibikaji kufuatia aibu iliyomkuta.

Alisema alikua amejipanga kufanya kila linalowezekana ili kutimiza lengo la kumaliza kiu ya mashabiki wa soka nchini England kwa kuifikisha mbali timu hiyo, lakini hatua ya kushindwa anaiona kama sehemu iliyompa msukumo wa kuamini kazi yake ina ulazima wa kuishia hapo alipofikia.

“Ninawataka radhi wale wote waliokwazika na matokeo haya, na mimi sina budi kujiuzulu nafasi yangu,”

“Ninatarajia mtaiona England nyingine tofauti na hii niliyokua nayo mimi na itafanikiwa kufika mbali ikiwa na mtu mwingine atakaekuja badala yangu.” Alisema Hodgson

Hodgson, alikabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi cha England, mwaka 2012, baada ya kujiuzulu kwa Fabio Capello.

Katika utawala wake, Hodgson amekiongoza kikosi cha England kwenye michezo 56 na amefanikiwa kushinda michezo 33 pekee.

Nampalys Mendy Kukabidhiwa Mikoba Ya Kante
Marekani: Bado Tunaitafakari Uingereza