Serikali kupitia Wizara ya afya, ipo kwenye ufuatiliaji kuhakikisha watu wanapata chanjo kamili ya Uviko-19 kutokana na takwimu kuonesha watu 1,648,219 kati ya 8,599,228 waliochoma chanjo ya Pfizer na Sinopharm katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti 14 hawapata chanjo ya pili.

Mratibu wa Elimu kwa Umma na Ushirikishaji Jamii wakati wa dharura (RCCE), wa Wizara ya Afya, Juliana Mshama ameyasema hayo na kudai kuwa kipindi cha mwezi Julai, watu 1,712,107 walichoma chanjo ya Pfizer na kati yao 449,416 sawa na asilimia 26 hawakurudi kwa ajili ya dozi ya pili kama inavyotakiwa.

Amesema, “kati ya watu 2,439,250 waliopata chanjo ya Sinopharm watu 325,982 sawa na asilimia 13 hawajarejea kupata dozi ya mwisho na katika kipindi cha Agosti Mosi hadi 14, watu 416,869 kati watu 1,719,296 walichoma chanjo ya Pfizer sawa na asilimia 24 ya waliotakiwa kurudi hawakufanya hivyo.”

Muonekano wa chanjo ya Pfizer.

Aidha, katika kipindi hicho watu 455,952 kati ya watu 2,728,575 waliopata chanjo ya Sinopham ambayo ni sawa na asilimia 17 pia hawajarudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Sinopharm huku akisema lengo la serikali ni kuchanja watanzania 59,744 wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea kwa siku.

Hata hivyo, idadi ya watu waliopata chanjo kamili tangu ilipozinduliwa Julai 28, 2021 ni 15,960,643 ambayo ni sawa na asilimia 51.92 ya wananchi zaidi ya milioni 30.74 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea waliokusudiwa kupatiwa chanjo hiyo.

Takwimu za Wizara ya Afya, zinaonesha kuwa wanaume waliopata chanjo tangu zilipoanza kutolewa Tanzania bara ni asilimia 54 huku wanawake wakiwa na wastani wa asilimia 46 ambapo bado Serikali inahimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Mshama amesema, Mikoa ya Arusha, Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam ni vinara kwa wakazi wake kupata chanjo kwa asilimia 85, na kwamba mikoa iliyo chini ya asilimia 50 ya watu wake kupata chanjo Iringa, Songwe, Singida, Katavi, Rukwa na Pwani.

Waziri Mkuu ahudhuria Mkutano TICAD
Kenya: Moto waiwakia IEBC kesi matokeo ya urais