Kwa kiasi kikubwa nguzo za uchumi wa Kenya, mbali na utalii, ni kupakana kwa taifa hilo na Bahari ya Hindi na kuifanya Bandari ya Mombasa kuwa lango kuu la biashara kimataifa.

Miezi michache iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta, amezindua bandari nyingine kubwa na ya kisasa mwambao wa Bahari ya Hindi; Bandari ya Lamu, hivyo kujihakikishia ufalme katika masuala ya uingizaji mizigo eneo la Afrika Mashariki.

Maofisa wa juu wa Bandari ya Mombasa wamewahi kutembelea Tanzania na katika masuala yaliyowatia hofu ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, wakiamini kuwa mipango iliyokuwa imewekwa ingeifanya bandari hiyo kuwa kubwa na ya aina yake katika mwambao wote wa mashariki ya Afrika.

“Ni bahati mbaya kwa Tanzania lakini ni neema kwa Kenya kwamba hadi leo bandari hiyo haijaanza kujengwa, hivyo kuwapa majirani zetu miaka kadhaa ya kutamba kibiashara,” anasema mfanyabiashara wa Bagamoyo, Mohamed Abood Saleh.

Hata hivyo, miaka hiyo ya Kenya kutamba sasa inahesabika kwa kuwa zipo dalili kuwa bandari hiyo itaanza kujengwa wakati wowote katika utawala wa Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mfanyabiashara huyo anasema: “Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu sana mjadala wa suala hili kwa miaka miwili – mitatu iliyopita. Ninayafahamu mengi, pia nimejifunza mengi, kwa kuwa nimesoma nyaraka nyingi pia.

“Hapa nitakupa sehemu ya waraka mmoja ulionipendeza sana kuhusu suala hili, kwa kuwa umechimba historia yake kwa undani na kuibuka na ‘nyundo’ za kupendeza.

“Kwetu sisi wakazi wa Bagamoyo tunaamini ujenzi huu ukikamilika, fursa zitafunguka na maendeleo ya kweli yatapatikana katika kipande hiki cha ardhi ya Tanzania na kutapakaa nchi nzima kama ilivyokuwa katika ustaarabu wa Uislamu na Ukristo kutapakaa kutokea Bagamoyo.

“Sasa hebu fuatilia waraka huu tujifunze kwa pamoja umuhimu wa kuwapo kwa Bandari ya Bagamoyo. Unaosomeka hivi:

“Mradi huu ulibuniwa na serikali chini ya ‘Bagamoyo Special Economic Zone Project’ mwaka 2004; mpango kabambe wa ujenzi wa sekta mpya ya viwanda. Japan ndiyo ilitusaidia kwenye hili. Mradi huu uliitwa ‘Tanzania-Mini Tiger 2020’ ndani ya Wizara ya Viwanda.

“Tulisikia kwamba Mamlaka ya Bandari (TPA) ilibuni mpango wa miaka 20 wa uendelezwaji wa bandari nchiniu (The Tanzania Port Development Master Plan 2009 – 2028).

“Mpango huo ulipendekeza Bandari ya Bagamoyo ijengwe na iwe tayari mwaka 2021/2022 kujaza nafasi baada ya Bandari ya Dar es Salaam kufikia ukomo wa kuweza kuongezewa uwezo.

“Kwa hiyo mambo mawili ya msingi hapa ni kwamba; kwanza, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo tuliubuni sisi wenyewe, ulikuwa sehemu ya mipango yetu ya muda mrefu na haukujengwa kwa msukumo wa Wachina.

“Pili, huu si mradi wa bandari pekee, bali ni mradi wa ukanda wa kiuchumi unaoendana na mji wa viwanda.

“Mwaka 2009, TPA kupitia Kampuni ya Hamburg Port Consulting ya Ujerumani, ilifanya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na kuona una manufaa ukitekelezwa.

“Mwaka 2011, Wizara ya Viwanda na Biashara, kupitia CowiConsult, nayo ilifanya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone (BSEZ), kwa kufungamanishwa na Mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

“Mipango yote hii ilikuwa ni yetu wenyewe, na tulijiridhisha kama nchi kwamba Bandari ya Bagamoyo tunaihitaji na tukaiweka kwenye Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa kama mradi wa taifa wa kielelezo.

“Mwaka 2013 na 2014, Kampuni ya China Merchants Ports Limited, ikiungana na Mamlaka/Mfuko wa Uwekezaji wa Oman (OIA), waliomba kuwekeza BSEZ na Bandari ya Bagamoyo.

“Baadaye kidogo, Korea Kusini nao, kupitia taasisi yao ya Science and Technology Policy Institute (STEPI) ilikamilisha upembuzi yakinifu wa kuwekeza katika kujenga na kuendeleza Bagamoyo High Technology Park kwa kushirikiana na EPZA na COSTECH.

“Kwa hiyo hoja nyingine ya kuzingatia hapa ni kwamba Bagamoyo si uwekezaji wa Wachina pekee kama inavyodhaniwa. Yapo mataifa mengine. Oman wanaweka fedha yao nyingi hapa. Korea Kusini nao wanaweka pesa na maarifa yao.

“Kama nilivyoeleza hapo awali, kwa mujibu wa Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo (FYDP II), BSEZ ni mradi wa taifa wa kielelezo unaotarajiwa kuvutia uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 10!

“Utakuwa na viwanda 760 na hatimaye kutoa ajira 270,000 kwa awamu ya kwanza. Majadiliano ya utatu wa Tanzania, China Merchants na Oman yalikuwa yanaendelea kuelekea makubaliano na hatimaye kuingia mikataba ya uwekezaji kabla ya kusimamishwa.

“Zipo hoja kubwa tatu zinazosemwa kuhusu mradi huu: kwanza, utatutwika madeni kama Kenya na Sri Lanka, ambako Wachina walilazimika kutaifisha bandari; pili, tutaua Bandari ya Dar es Salaam; tatu, haturuhusiwi kuendeleza bandari yoyote na haturuhusiwi kutia mguu Bagamoyo kwa miaka 99!

“Hoja hizi zote si za kweli, na kwa kweli wawekezaji wa huu mradi wamekuwa wakipambana kutafuta namna ya kuzijibu bila mafanikio.

“Wawekezaji hawa, hasa wa Oman, ni mamlaka za serikali na wasingependa malumbano, hasa na Serikali ya Tanzania.

“Hoja ya kwanza, kwamba tutakopa na kujitwika deni kubwa si ya kweli, kwa kuwa kwenye mradi huu hakuna hata senti tano ya mkopo! Huu ni uwekezaji. Hakuna deni hapa, ni pesa ya kigeni inaingia kuwekezwa.

“Hoja ya pili kwamba tutaua Bandari ya Dar es Salaam haina mantiki, kwa sababu hata kabla Wachina hawajafika, ilikuwa ni ndoto na mipango ya TPA kujenga Bandari ya Bagamoyo.

“Ukisoma Mpango Kabambe wa Miaka 20 wa Uendelezwaji wa Bandari za Tanzania (The Tanzania Port Development Master Plan 2009 -2028), TPA wenyewe walitaka Bandari ya Bagamoyo iwe imejengwa ifikapo mwaka 2023. Bandari za Bagamoyo na Dar es Salaam si bandari shindani.

“Ni bandari zitakazosaidiana kuongeza shehena ya mzigo unaopita nchini. Basi! Pia Bandari ya Bagamoyo itajengwa kwa kuzingatia teknolojia ya uundwaji wa meli za kisasa (4th Generation Shipbuilding Technology Port).

“Meli hizi ambazo zitakuwa zinaongezeka kadiri miaka inavyokwenda, haziwezi kutia nanga kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Na kama unaitazama nchi kwa miaka 50 hadi 100 ijayo, Bandari ya Dar es Salaam ina ukomo wa upanuzi. Lazima kama nchi ni muhimu kujenga bandari mpya kubwa katika ukanda huu ili kuendelea kunufaika na faida ya kijiografia.

“Hoja ya tatu kwamba Wachina wanataka tusijenge wala kuendeleza bandari nyingine yoyote kwa miaka 99 na tuwape bandari hiyo bila kutia mguu pale, si kweli. Hakuna pahala popote wawekezaji wametoa madai hayo.

“Ukweli ni kwamba kote duniani mwekezaji anapoweka fedha zake mwenyewe kwenye mradi, atataka muda wa kutengeneza faida kabla hajakukabidhi mradi. Hapa Wachina na Wa-Oman walitaka miaka 33 ya concession.

“Je, ni mingi au ni michache? Inategemea fedha iliyowekwa (dola za Marekani bilioni 10) na standard practice kwingine duniani.

“Reli ya kuunganisha UK na Ufaransa, ambayo imejengwa na sekta binafsi ina concession ya miaka 50. Kwa bandari, standard practice ni miaka 25 – 40, kutegemeana na ukubwa wa uwekezaji.

“Cha msingi kwa timu yetu ya majadiliano ni kupata financial models wa wawekezaji na kuzichambua na kuona wanaanza kupata faida baada ya muda gani.

“Na cha kutambua pia ni kwamba concession inahusu tu faida ya bandari na kwamba katika kipindi hiki cha concession bado TRA itakuwa inakusanya kodi nyingine zote husika za mizigo bandarini.

“Suala jingine la kutazama katika kufanya uamuzi ni kuangalia dunia inaelekea wapi kwenye biashara ya kimataifa. Tutake tusitake, nchi yetu inategemea biashara ya nje kimapato na China kwa sasa ndiyo kinara wa biashara ya import and exports duniani.

“Inaongoza kwa kuagiza na kuuza bidhaa nje na itaendelea kuwa kinara kwa miaka 50 ijayo. Ukifungamana nao, utashinda. Kwa mujibu mpango wa China wa Belt-and-Road-Initiative (BRI), meli kubwa za bidhaa zitakazopita katika 21st Century Maritime Silk Road kusafirisha bidhaa kati ya China, Afrika ya Kati na Kusini, zitapita katika moja ya bandari za mwambao wa Afrika Mashariki.

“Hapo ndipo patakuwa lango kuu la kupokea, kuhifadhi kwa muda na kusafirisha shehena kwa meli au usafiri wa nchi kavu. Kulingana na kudra ya kijiografia ya Tanzania ambayo inaimarishwa na uwepo wa Reli ya Kati ya Kisasa (SGR) tunayojenga pamoja na reli ya TAZARA, Bandari ya Bagamoyo ambayo itaunganishwa na reli hizo, itakuwa haina mshindani nje ya Tanzania.

“Hii ni katika dhana nzima ya ushirikiano wa maendeleo ya uchumi baina ya China na Afrika, kupitia BRI kwa muktadha wa 21st Century Maritime Silk Road.

“Mwisho, ni muhimu kutambua kwamba kuna siasa za ushindani na majirani zetu kwenye hili suala. Jirani zetu wa kaskazini wanapigana kufa au kupona mradi huu usitokee. Kwa hiyo mtaona upotoshaji mwingi wa habari kuhusu huu mradi huku baadhi ya watu wetu wakitumika bila kujijua.

“Wenzetu tayari wameanza tena kuifuata Kampuni ya China Merchant kuwashawishi wahamishie mradi kule Lamu, Kenya. Mwaka 2018 wakati wa mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), kiongozi wao alikwenda Shenzhen, China kuwashawishi waende kwao.

“Bahati njema kwetu China Merchant walikataa na ndipo wakakutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Majuzi, Machi 25 mwaka huu, majirani zetu hawa wameandika barua tena kwa China Merchant kuomba mradi upelekwe kwao! Ni vita na mapambano.

“Namalizia kwa hadithi ndogo: mwaka 1970, wakati Dubai bado ni kamji kadogo jangwani, Wazungu waliona potential ya location yake kibiashara na wakamwendea mfalme wa wakati huo, Rashid bin Saeed Al Maktoum kupendekeza wajenge bandari na waiendeshe kwa miaka 30.

“Washauri wake wakamwambia; ‘tusiwape Wazungu bandari kwenye nchi yetu’. Sheikh akawauliza; ‘sisi tuna pesa ya kujenga?’ wakajibu; ‘hapana’, akawauliza; ‘tutaipata lini?’ wakasema; ‘hatujui’, akawauliza; ‘Dubai itaendelea kuwepo miaka 30 ijayo?’ wakajibu; ‘ndiyo’, akawauliza; ‘baada ya miaka 30 wataing’oa bandari na kuondoka nayo?’ wakajibu; ‘hapana’, akasema; ‘tuwape’.

“Wazungu wakajenga Port Rashid mwaka 1972. Miaka 30 ikapita haraka. Watu wa Dubai wakajenga uwezo wa kuendesha bandari na wakaanzisha Dubai Port World (DP World), moja ya kampuni kubwa duniani.

“Dubai sasa ni kinara wa bandari duniani. Majuzi wamechukua bandari za Senegal na Angola. Na wamejenga bandari hadi Rwanda ambapo hakuna hata bahari! Wanawasaidia Rwanda kwenye biashara ya usafirishaji.

“Mpendwa wetu Rais John Magufuli, alipenda maendeleo. Alitaka nchi yetu ipate manufaa kwenye miradi na mikataba. Namna ya kumuenzi ni kufanya makubaliano yenye tija kwa taifa katika Mradi wa Bandari ya Bagamoyo. Na hilo linawezekana kama timu yetu ya majadiliano itakuwa makini kuzingatia masilahi ya nchi.”

Arafat amkataa Ajib mazima
Maneno ya Niyonzima baada ya kuagwa Young Africans