Bodi ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imekubali kuipa Tanzania dola za Marekani milioni 567.25 (Sh1.3 trilioni) ambazo ni msaada wa dharura kwa ajili ya kushughulikia janga la Uviko-19.

Fedha hizo zinajumuisha mkopo nafuu usio na riba kupitia dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) wa jumla ya dola za Marekani milioni 189.08; na mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha la Rapid Financing Instrument (RFI) wa dola za Marekani milioni 378.17.

Sekta zitakazonufaika kulingana na makubaliano na IMF ni afya, elimu, utalii, maji, pamoja na kusaidia kaya maskini kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii (TASAF) na kuwezesha makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Kila sekta itatumia fedha hizo kwenye masuala yanayolenga kukabiliana na na athari za UVIKO-19 ambapo pamoja na mambo mengine, Sekta ya afya itanunua dawa na vifaa tiba vya kupambana na UVIKO-19 na kugharamia utekelezaji wa mpango wa chanjo.

Sekta ya elimu itaweka mazingira yatakayowezesha wanafunzi kujifunza bila msongamano na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maboma ya shule na kuongeza madawati.

Mtazamo wa uchumi wa Tanzania umedorora kutokana na athari za janga la Uviko-19 pamoja na kuanguka kwa utalii baada ya vizuizi vya kusafiri, uchumi unaripotiwa kupungua kwa ukuaji wa asilimia 4.8 mwaka 2020, na ukuaji unatarajiwa kubaki chini kwa mwaka 2021.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Serikali imeonyesha nia kwa kufuata sera za uchumi zinazofaa kushughulikia athari za janga hilo na kujitolea kuimarisha uratibu na uwazi ili kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinatumika katika kupambana na janga hilo.

Watano wafariki kwa ajali Arusha
John Bocco amsikitisha Kim Poulsen