Mlinda mlango kutoka nchini Urusi/Russia Igor Akinfeev, ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo aliyoiongoza kama nahodha wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2018.

Akinfeev mwenye umri wa miaka 32, amechukua maamuzi hayo kwa kuamini kuwa ni muda sahihi wa kufanya hivyo, ambapo kwa sasa kikosi cha Urusi kinaendelea na mchakato wa kusaka ubingwa wa michuano ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA Nations League).

Mlinda mlango huyo wa klabu ya CSKA Moscow inayoshiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya, amesema maamuzi ya kustaafu soka la kimataifa (Timu ya taifa) aliyadhamiria siku nyingi na alichokua anasubiri ni muda wa kufanya hivyo.

“Nilidhamiria kuchukua hatua hii tangu tulipomaliza fainali za kombe la dunia, lakini nilikua natafuta siku maalum ya kuwatangazia wadau wa soka wa Urusi na kwingineko duniani.

“Nimefanya mengi nikiwa na timu ya taifa, ninaamini nimejitahidi kwa uwezo wangu, ninaamini atakaekuja badala yangu atafanya viziri zaidi,” Akinfeev alisema kupitia tovuti ya klabu ya CSKA Moscow.

Mpaka anatangaza kustaafu, Akinfeev tayari ameshacheza michezo 112 akiwa na timu ya taifa ya Urusi ambayo kwa mara ya kwanza aliitumikia mwaka 2004, akiwa na umri wa miaka 18.

Kuhusu mafanikio ya kucheza kwa mara ya kwanza hatua ya robo fainali ya kombe la dunia, huku akiwa mmoja wa waliowezesha jambo hilo, Akinfeev amesema anajihisi faraja kwa sababu anaamini mashabiki wa soka nchini humo walisubiri kwa muda mrefu.

“Ni hatua kubwa sana katika historia ya maisha yangu ya soka, nimefanikiwa kuwa miongoni mwa wachezaji walioiweka Urusi kwenye ramani ya soka, kupitia fainali za kombe la dunia zilizochezwa hapa nyumbani,” alisema.

“Kwa kweli sikuwa na ndoto za kufikia hatua hiyo, kwani wapo wazuri na wenye uwezo walishindwa miaka ya nyuma, lakini nimekua miongoni mwa walioweza kufika hatua ya robo fainali, kwa hilo namshukuru mungu na kila mmoja aliyekua nasi.”

Urusi ilitoewa na Croatia katika mchezo wa robo fainali wa kombe la dunia kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4 kwa 3.

Taifa Stars yaanza kuiwinda Cape Verde
Diamond arejea kuokoa maisha ya Hawa, ampa mamilioni