Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema kuwa Jeshi hilo litafanya uchunguzi kuhusu mambo kadhaa yaliyoelezwa mitandaoni kuhusu sababu za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Media, Dkt Reginald Mengi na kwamba kama kweli kimesababishwa na mtu sheria itachukua mkondo wake.

Akizungumza na vyombo vya habari alipofika nyumbani kwa marehemu, Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuifariji familia, IGP Sirro ameeleza kuwa amekuwa akifuatilia mitandao ya kijamii na ameona mengi yaliyoenezwa hivyo jeshi hilo halitayapuuzia.

“Hili suala la mitandao nimelisikia sana, na nafuatilia sana mitandao. Niseme tumelichukua, wananchi watulie. Tumalize kwanza msiba halafu tufuatilie haya yanayowesemwa yana ukweli kiasi gani, kama kuna mkono wa mtu sheria itachukua mkondo wake, kama haitakuwa mkono wa mtu basi ni kitakuwa ni kifo chakawaida,” amesema IGP Sirro.

“Na sisi tayari tumeshafungua kadokezo ketu ka kuona haya yana ukweli kiasi gani tufuatilie tuone kama kweli kuna mkono wa mtu sheria itachukua mkondo wake, siku zote tunasema hakuna mtu aliye juu ya sheria lakini pia hatuwezi kumuonea mtu juu ya mitandao sababu yanapotokea mambo ya namna hii wale walio na chuki wanapata nafasi ya kusema maneno sisi kama jeshi hatupuuzi jambo la msingi ni kutafuta ushaidi kupata ukweli” ameongeza.

Sirro amesema Dkt. Mengi ni miongoni mwa matajiri waliokuwa wanafanya kazi kwa ukaribu sana na jeshi la polisi hivyo ameomba jeshi la polisi na wananchi kutimiza wajibu wao ili kuleta amani kama ambavyo Dkt. Mengi amekuwa akisisitiza.

Aidha amesema jeshi la polisi kwa ujumla limempoteza mshauri kwani Mengi alikuwa moja ya mshauri mkubwa kwa mambo mengi yaliyokuwa yakiendelea jeshi la polisi.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa jeshi hilo linamkumbuka Dkt. Mengi kwa mchango mkubwa na ukaribu aliokuwa nao kwa vyombo vya usalama, na kwamba hivi karibuni alishiriki katika tukio la kutoa zawadi kwa askari wa jeshi hilo jijini humo.

Dkt. Mengi alifariki usiku wa kuamkia Mei 2, 2019 akiwa Dubai alipokwenda kwa ajili ya mapumziko. Mwili wake unatarajiwa kufika nchini Jumatatu ya Mei 6 kwa ajili ya taratibu nyingine za heshima ya mwisho na hatimaye mazishi yatakayofanyika nyumbani kwao, Machame-Moshi.

Wanaume wanaonyanyaswa na wake watakiwa kufunguka
Ferooz: Wanatumia uchawi kumbomoa msanii watengeneze brand zao

Comments

comments