Mkuu wa Jeshi la polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema ndani ya gari lililotumika kumteka mfanyabiashara Mo Dewji lenye namba za usajili T314 AXX limekutwa na silaha 4, risasi 19 za AK 47 pamoja na pisto 3.

IGP Sirro amezungumza hayo mapema leo pindi alipoitisha vyombo vya habari kuzungumza sakata la kupatikana kwa Mo ambapo ameachiwa alfajiri ya leo na kutelekezwa katika eneo la Gymkhana ambapo familia ya Mo ilimkuta hapo.

”Waliomteka walikuwa na silaha moja ya kivita na pisto 3, ambapo silaha hiyo ya AK 47 ilikuwa na risasi 19 ni  silaha ya kivita iko vizuri na inapiga, ni moja ya silaha iliyokutwa ndani ya hiyo gari, na magazine yake ”Amesema Sirro.

Aidha IGP Sirro amesema Mo yupo salama na upelelezi kwa kina unaendelea kuhakikisha waliomteka wanapatikana.

Sirro ameomba ushirikiano kutoka kwa wananchi kwani tayari hatua waliyofikia ya kulikamata gari pamoja na silaha zilizotumika katika utekaji ni viashiria vizuri kuwa hivi karibuni watekaji hao ambao ni watu wasiojulikana watatiwa mbaroni.

Mo alitekwa mnamo Oktoba 11, 2018 katika hoteli ya Collosseum ambapo alikwenda kufanya mazoezi, ndipo watekaji hao walifyatua risasi juu na kumchukua kinguvu Mfanyabiashara huyo.

Mo amekaa mateka kwa takribani siku 10 sawa na wiki moja na siku 3, hatua iliyojenga hofu kwa familia na kudiriki kutangaza dau la kitita cha fedha Bilioni 1 kwa mtanzania atakayesaidia kutoa taarifa za upatikanaji wake.

Tanzia: Bongo muvi yampoteza mmoja, afariki dunia
Umoja wa Mataifa watangaza vita dhidi ya upimaji ubikira