Benchi la Ufundi la Ihefu FC limeanza kazi ya kujipanga na mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Simba SC utakaopigwa jijini Dar es salaam Aprili 7.

Simba SC na Ihefu FC zinatarajia kukutana mara mbili Aprili zikianza na mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC utakaopigwa jijini Dar es Salaam na siku chache kuvaana katika Ligi Kuu Bara mkoani Mbeya.

Kocha Msaidizi wa Ihefu FC, Zuberi Katwila amesema walitoa mapumziko kwa timu na sasa wamerudi kambini kwa ajili ya kujiandaa na michezo hiyo miwili ndani ya mwezi mmoja ambayo yote amekiri kuwa ni muhimu kwao.

“Tuna dakika 180 ngumu tunahitaji kujiandaa mapema kwa kujiweka fiti kutokana na kukutana na wapinzani ambao wamepata wakati mzuri wa kucheza michezo mingi mfululizo katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wanayoshiriki na sisi tulikuwa na mapumziko kupisha michezo miwili ya timu ya taifa.”

“Kwa asilimia kubwa kikosi kipo ni wachezaji wachache walioitwa timu za taifa hivyo tutaendelea kujiweka fiti ili muda ukifika timu inakuwa bora ikiwa ni pamoja na wachezaji kuandaliwa kisaikolojia kuhakikisha wanatumia kila nafasi watakayotengeneza ili kuweza kujiweka nafasi nzuri,” amesema Katwila.

Katwila amesema kikosi kimeimarika baada ya wachezaji kuingia kwenye mfumo na wameanza kuona utofauti na malengo yao yanaenda kutimia kutoka kuwa kwenye presha ya kushuka daraja na sasa kuwania tano bora kwenye msimamo.

Amesema ubora uliopo kwenye kikosi chao hawataki kuona unaanza kupotea kutokana na kutokukaa pamoja kwa muda mrefu ndio maana wamewarudisha wachezaji haraka kambini ili kuendelea kuwaweka kwenye hali ya ushindani.

Amrouche: Hatuna sababu za kupoteza mchezo
Mahmoud Kahraba amaliza utawala wa Chama