Ikulu ya Tanzania imekanusha kupokea maombi yoyote ya mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kutaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete kujadili mgogoro wa matokeo ya Zanzibar.

Ikulu imeeleza kuwa haijawahi kupokea maombi yoyote kutoka kwa mwanasiasa huyo wakati wa uchaguzi na hata baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

Hata hivyo, kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Ikulu imeeleza kuwa Rais Kikwete alipokea nakala ya malalamiko ya Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusu vitendo vya baadhi ya polisi visiwani Zanzibar pamoja na ombi la kuwezesha mazungumzo kati ya Maalim Seif Sharif Hamad kufanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Mwamunyange.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais Kikwete alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu kufanya uchunguzi juu ya malalamiko hayo na kumpatia taarifa kamili pamoja na kuwezesha mazungumzo kati ya Mkuu wa Majeshi na Viongozi wa CUF. Ilieleza kuwa Rais Kikwete yuko tayari kutoa ushirikiano kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa uchaguzi visiwani Zanzibar.

Jana, Maalim Seif alieleza kuwa amefanya jitihada za kuwasiliana na Rais Kikwete kwa njia ya simu lakini jitihada hizi zilishindikana kutokana na kutopewa ushirikiano na wasaidizi wa Rais.

 

Kafulila: Sikuibiwa Kura, Nilinyang’anywa Ushindi Kwa Nguvu
Maalim Seif Ataja Siku Ya Mwisho Ya Kuwaomba ZEC Na Hatua Atakayochukua