Nyota wa zamani wa Kriketi kutoka nchini Pakistani, Imran Khan anaongoza katika kura za uchaguzi mkuu wa nchi hiyo huku matokeo yakicheleweshwa kutangazwa.

Baadhi ya wapiga kura wameyakataa matokeo kabla hata ya kutangazwa wakidai kuwa yamecheleweshwa kwa makusudi.

Wafuasi wa chama cha Tehreek-e-Insaf (PTI) cha mchezaji wa zamani wa kriketi Imran Khan wameonekana wakishangilia ushindi wa mgombea wao ingawa ni asilimia 48 tu ya kura ambazo tayari zimeshahesabiwa hadi sasa kutokana na kucheleweshwa kwa zoezi hilo.

Tume ya Uchaguzi ya Pakistani (ECP) imesema kuwa mchakato wa kuhesabu kura umecheleweshwa kutokana na sababu za kiufundi, huku ikikataa madai ya udanganyifu.

Aidha, akizungumza na vyombo vya habari, Katibu wa tume hiyo, Babar Yakoob amesema kuwa kuchelewa huko kumetokana na kuharibika kwa mfumo wa utoaji matokeo wa (RTS) ambao umeanza kutumika kwa mara ya kwanza katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, kulingana na matokeo yasiyo rasmi yaliyotangazwa na vyombo vya habari vya ndani ya nchi, chama cha Tehreek-e-Insaf (PTI) cha Khan ambacho kinadaiwa kuungwa mkono na jeshi la nchi hiyo, kimepata asilimia kubwa ya kura huku chama cha Sharif kikiwa kimeshika nafasi ya pili.

 

 

Dkt. Kigwangalla awawashia moto waliovamia Pori la Akiba
Picha: Miss Ilala, Dar24 Media wafanya ziara mashuleni