Kwa mara ya kwanza katika historia ya soka Tanzania, vigogo wa juu katika Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa na lile la Afrika, CAF wamekutana katika mkutano maalumu kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya soka.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino alisema kuwa mkutano huo uliokuwa wa mafanikio, umeshirikisha nchi wanachama 19 za FIFA, na ulikuwa wa mafanikio.

Mkutano huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) unajulikana kwa jina la  “Fifa Executive Football Summit”.

Katika mataifa hayo 19, yaliwakilishwa na Rais na Katibu wake mkuu.

Tanzania ni  nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyopewa heshima ya kuandaa mkutano huo ambao pia ulijadili masuala  ya soka la wanawake, vijana na mfumo wa usajili wa kielektroniki wa TMS ambao kwa sasa utakuwa chini ya FIFA wenyewe na si wakala.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi mkubwa wa Fifa kutembelea Tanzania na kubwa zaidi ni kupewa nafasi ya mkutano wa siku moja ambao viongozi wa mashirikisho ya soka katika nchi mbalimbali walishiriki.

Rais Infantino alisema madhumuni hasa ya mkutano huo ni kuirejesha Fifa kwenye mpira wa miguu na mpira wa miguu kwa FIFA, kupanga mikakati ya maendeleo  ya siku za usoni ikiwa ni pamoja na mataifa 12 duniani kupewa heshima ya kuandaa mikutano hiyo.

Infantino alisema pia kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni kutokana na uongozi bora wa TFF na ni kuwatia moyo kufanya vizuri zaidi katika kuusimamia mchezo huo.

Pia alisema Fifa inaanza kuondokana na kufanyia mikutano Zurich na itakuwa ikiisogeza kwa wanachama wake ikiwemo Tanzania na ndiyo maana mkutano huo umefanyika Dar es Salaam.

Infantino alisema pia kuwa hiyo itasaidia katika mapambano ya rushwa ndani ya vyama na mashirikisho ya soka.

“Tanzania iko kwenye kampeni dhidi ya rushwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye michezo, lakini pia huo ni mkakati wa FIFA katika mapambano dhidi ya rushwa katika soka,” alisema.

Simba wapewa mbinu za kuimaliza Al Masry kwa Dk 90
Taarifa kutoka RT, wakubali agizo la BMT

Comments

comments