Kiungo kutoka nchini Hispania Hispania Andres Iniesta amesema anaachana na klabu yake ya Vissel Kobe baada ya kuitumikia kwa miaka mitano, huku akitaja sababu ya kukosa nafasi ya kucheza kuwa chanzo cha kuchukua uamuzi wa kuondoka japo hajaamua kustaafu soka.

Iniesta, ambaye alishinda Kombe la Dunia na timu ya taifa ya Hispania mwaka 2010, mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji tisa ya Ligi Kuu ya Hispania na FC Barcelona, alitokwa na machozi alipotangaza kuachana na klabu hiyo.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 39, aliingia kwenye mechi tatu tu msimu huu lakini alisema amepanga kuendelea kucheza soka ingawa hajaweka wazi kwenye timu gani.

Alipoulizwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari wapi anatarajia kuelekea, Iniesta alisema: “Lazima niwaambie ukweli, sijui wapi.

“Nataka kuendelea kucheza soka. Nahisi bado nina uwezo wa kuendelea kucheza. Lakini ukurasa huu nimeufunga, tutaona nini kinawezekana. Nataka kumaliza maisha yangu ya soka uwanjani na hicho ndicho natazamia.”

Baada ya kumaliza maisha yake ya soka yaliyodumu kwa muda mrefu katika klabu ya Barcelona, Iniesta alijiunga na klabu hiyo ya Japan mwaka 2018 kwa mkataba wa miaka mitatu na kuongeza mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu hiyo.

Mechi ya mwisho kwa fundi huyo wa mpira inatarajia kuwa Julai Mosi. Vissel timu anayoitumikia nyota huyo inaongoza Ligi Kuu ya Japan baada ya raundi 14 katika ligi hiyo. “Ni siku ya hisia baada ya miaka mingi sana,” aliongeza.

“Nilijaribu kutoa kila liwezekanalo ndani na nje ya uwanja. Najivunia kwenye hilo.”

Iniesta alifunga bao la ushindi katika muda wa nyongeza kwenye mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi ambapo Hispania iliibuka na ushindi  wa bao 1-0 na kunyakua taji hilo.

Kiungo huyo mkongwe alisema uamuzi wa kwenda kucheza soka Japan ni uamuzi bora aliowahi kufanya katika maisha yake.

Arme Slot aikataa Tottenham Hotspur hadharani
Waaswa usafi wa mwili, Mazingira kukabili magonjwa ya mlipuko