Klabu ya Inter Milan ya nchini Italia, huenda ikafanikiwa kumnasa kiungo kutoka nchini Ivory Coast na klabu ya Manchester City, Yaya Toure baada ya kuripotiwa kutenga fungu la kutosha ambalo litatumika kwenye harakati za kumuhamisha kutoka nchini England.

Wakala wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, Dimitri Seluk, tayari ameshaonyesha nia ya dhati ya kutaka kuona mchezaji wake anaondoka Etihad Stadium, kufuatia kigugumizi cha viongozi wa klabu ya Man city cha kuzungumzia suala la kumsainisha mkataba mpya.

Inter wanatajwa kuwa tayari kumlipa mshahara wa Euro million 5 kwa mwaka mchezaji huyo huku ikielezwa watamsainisha mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo upinzani mkali ambao huenda ukapatikana dhidi ya Inter Milan unatarajiwa kutoka katika ligi ya nchini China ambayo inaendelea kujizolea umaarufu kwa kuwasajili wachezaji wenye hadhi kubwa duniani, kutokana na baadhi ya klabu za nchi hiyo kuonyesha nia ya kumsajili Yaya.

Mpaka sasa klabu kutoka nchini China ambazo zina lengo la kumsajili kiungo huyo hazijajitokeza hadharani, lakini inasemekana zipo tayari kuingia katika vita ya kumuwania.

Toure anatajwa kuwa tayari kuondoka Man City kwa sababu mbili tofauti ambapo sababu ya kwanza ni ukimya wa kutosainishwa mkataba mpya huku nyingine ni kutokua na mahusiano mazuri na meneja mpya ambaye ataanza kazi mwishoni mwa msimu huu Pep Guardiola.

Ander Herrera: Tutamaliza Ligi Juu Ya Man City
Antonio Conte Kuanza Na Beki Wa Kitaliano