Kiongozi Mkuu wa Kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei ametoa ‘mawaidha’ yake ya Ijumaa ya kwanza tangu mwaka 2012 na kulitetea Jeshi la Mapinduzi la nchi hiyo kufuatia kudungua kimakosa ndege ya abiria ya Ukraine na kuua watu 176 waliokuwemo.

Ujumbe wa kiongozi huo umekuja ikiwa ni siku chache tangu Marekani ilipomuua kamanda wa Iran aliyekuwa nchini Iraq, Jenerali Qassem Soleimani na baadaye Iran kujibu kwa kushambulia kambi mbili za jeshi la Marekani. Kadhalika, Iran ilikiri kudungua ndege hiyo ya abiria ikieleza kuwa ilidunguliwa kimakosa kutokana na kudhaniwa kuwa ni hatari wakati wa taharuki iliyokuwepo. Ndege hiyo ilikuwa inaruka kutoka Tehran, Januari 8.

Khamenei alielezea kitendo hicho kama ‘janga lenye machungu’, na kueleza kuwa maadui wa Iran walitumia tukio hilo na hatua ya jeshi kukiri kufanya makosa kama silaha ya kutaka kulipunguzia nguvu Jeshi la Mapinduzi.

“Kuanguka kwa ndege hiyo kulikuwa ajali iliyotuumiza, ilichoma mioyo yetu sote,” alisema Khamenei. “Lakini wengine walitaka kuonesha taswira fulani ili watu wasahau kujitoa na kazi iliyofanywa na ‘Soleimani’,” aliongeza.

“Maadui zetu walikuwa na furaha kuhusu kuanguka kwa ndege ile wakati sisi tunahuzuni. Walifurahi kuwa wamepata kitu cha kuzungumza na kulihoji jeshi letu na mfumo wa Iran,” alisema.

Maelfu ya waumini walijumuika kwenye ibada hiyo iliyofanyika jijini Tehran kumsikiliza kiongozi mkuu, Khamenei. Walijaza maeneo yote na mitaa yote iliyokuwa nje ya jingo hilo na walipaza sauti zao, ‘Kifo kwa Marekani’.

Wiki iliyopita, Serikali ya Iran ilieleza kuwa watu kadhaa wanashikiliwa kutokana na kutunguliwa kwa ndege hiyo ya abiria. Rais wa Iran, Hassan Rouhani aliahidi kuwa kila aliyeshiriki kufanya kosa hilo ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.

Mbwana Samatta akamilisha vipimo kuingia Aston Villa, baba yake aeleza alichomwambia
Uchaguzi 2020: Dkt Bashiru awatumia salamu wapinzani, ataja karata ya ushindi