Iraq imesema kuwa majeshi yake yamefanya mashambulizi makali ya anga katika ardhi ya Syria yakilenga wapiganaji wa kundi la kigaidi linalojiita Islamic States of Syria and the Levant (ISIL au ISIS).

Tangazo la mashambulizi hayo limetolewa na waziri mkuu wa Iraq, Haider Al-Abadi ambaye aliwahi kuahidi kuwa nchi yake itafanya mashambulidhi dhidi ya kundi hilo katika eneo la Syria endapo litatishia usalama wake.

Ndege za kivita aina ya F-16 zimeshusha makombora katika eneo la mpaka wa Iraq na Syria mapema leo. Kwa mujibu wa ofisi ya Al- Abadi, mashambulizi hayo yalipata baraka kutoka Syria.

“Kwa kuzingatia amri kutoka kwa amiri jeshi mkuu, Haider al-Abadi, jeshi letu shujaa la anga limefanya mashambulizi makali dhidi ya ISIL katika eneo la Syria Alhamisi hii, karibu na mpaka wa Iraq,” imeeleza taarifa ya ofisi ya waziri mkuu huyo.

Al-Abadi aliwahi kutangaza ushindi dhidi ya kundi la ISIL nchini kwake mwaka jana kutokana na ushirikiano alioupata kutoka kwa majeshi ya Kurdish na Shia.

Hata hivyo, ISIL imeendelea kufanya mashambulizi ya kushtukiza katika baadhi ya maeneo ya Iraq hasa katika mpaka wa Syria na nchi hiyo.

Iraq ilitoa onyo kwa kundi hilo akiwataka kuondoka haraka katika maeneo ya mpaka wake na Syria kabla halijatekeleza mashambulizi ya anga.

Madhara ya mashambulizi hayo bado hayajawekwa wazi.

Comey adai Trump hashauriki
Swaziland sasa kuitwa eSwatin