Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni amesema kuwa nchi hiyo inaunga mkono juhudi za Tanzania katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona.

Amesema hayo jana, alipozungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi walipokutana na kufanya mazungumzo katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Waziri Kabudi alimfahamisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kwenye mapambano ya ugonjwa huo ambazo zimezingatia mazingiria na hali halisi ya Tanzania pamoja na nchi jirani zinazozunguka Tanzania.

Balozi Mengoni amepongeza juhudi hizo za Serikali
ambapo amefahamisha kuwa Serikali yake ya Italia inaziunga mkono na kwamba ipo tayari kutoa ushirikiano pale itakapohitajika kufanya hivyo.

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Kanali Wilbert Ibuge, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu mahusiano baina ya Tanzania na Italia.

Viongozi hao walikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa
kihistoria baina ya mataifa hayo mawili ambao umejikita katika sekta za elimu, afya, utalii pamoja na biashara na uwekezaji.

Live: Magufuli akigawa Tausi kwa marais wastaafu na Mjane mama Nyerere
Bodi ya mikopo yatoa Sh 63.83 bilioni kwa wanafunzi