Mtendaji mkuu wa klabu ya Arsenal Ivan Gazidis amewaomba mashabiki wanaompinga meneja Arsene Wenger, kubadili misimamo wao na kumuunga mkono babu huyo kutoka nchini Ufaransa.

Gazidis amewasilisha ombi hilo kwa mashabiki wa The Gunners, kwa kuwathibitishia Wenger atafanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa duniani.

Wenger, mwenye umri wa miaka 67, alisaini mkataba mpya wa miaka miwili mwezi uliopita, huku kukiwa na purukushani kwa baadhi ya mashabiki wanaompinga hadharani kwa kumtaka aondoke na kuwaachia klabu yao.

“Ninahitaji maelewano yawepo kati ya meneja na mashabiki wanaompinga, tunataka kuwa kitu kimoja, ili tufanikishe mipango tuliojiwekea kwa msimu mpya wa ligi kuu ya England,” Alisema Gazidis katika shughuli iliyomkutanisha na mashabiki.

“Tumekua tunashindwa kufikia malengo kwa madhaifu mengi likiwepo la kutokua wamoja, naamini muda umefika sasa, tumuonyeshe ushirikiano Wenger ili afanye kazi yake vizuri akianza na mpango wa usajili katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

“Ninawaomba sana, tuwe kitu kimoja na tumuonyeshe ushirikiano meneja wetu ili atuundie kikosi imara.”

Tayari Arsenal imeshafanya usajili wa beki wa pembeni kutoka Bosnia na Herzegovina Sead Kolasinac, huku ikiendelea kumfukuzia mshambuliaji wa kifaransa na klabu ya Olympic Lyon Alexandre Lacazette.

Kolasinac amejiunga na Arsenal, baada ya kumaliza mkataba wake na klabu ya Schalke 04 ya Ujerumani.

Wenger pia yupo kwenye mchakato wa kukamilisha mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya kiungo kutoka nchini Ujerumani Mesut Ozil, sambamba na mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Chile Alexis Sanchez.

Msanii Bobi Wine ashinda uchaguzi Uganda, kutinga Bungeni
Naibu Waziri afanya ziara ya kushtukiza mradi wa umeme Kinyerezi II, atoa agizo