Kiungo kutoka nchini Croatia na klabu ya Barcelona, Ivan Rakitic amesema haoni wa kumshinda Luka Modric katika kinyang’anyiro cha tuzo ya mchezaji bora wa dinia wa FIFA, baada ya orodha ya mwisho kutolewa juma lililopita.

Kiungo Modric anaeitumikia klabu ya Real Madrid ya Hispania, ametajwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA kwa kuchuana na Cristiano Ronaldo wa Juventus FC na Mohamed Salah wa Liverpool.

Rakitic amesema Modric amefanya makuba katika msimu wa soka wa 2017/18 akilinganisha na wanaoshindana naye, hivyo halitokua jambo la kutafakari kwa kiwango kikubwa kichwani mwake, zaidi ya kuamini Modric ndiye mshindi.

Tayari Modric ameshatangazwa kuwa mchezaji bora wa Ulaya (UEFA’s Player of the Year award) na kutajwa kwake kwenye orodha ya mwisho ya wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa FIFA, kumemuaminisha Rakitic kuwa ni sehemu ya mafanikio mengine kwa nahodha huyo wa Croatia kwa mwaka huu 2018.

“Kuna sababu nyingi sana ambazo zinampa ushindi Modric mpaka sasa, nikizielezea hapa sitazimaliza, lakini binafsi ninaamini mshindi ni huyu jamaa ambaye ni mtu anaependa kushirikiana na wengine wakati wote,” amesema Rakitic.

“Japo katika ushindani lolote linaweza kutokea, lakini kwa vigezo vinavyotumiwa na wapiga kura, sioni wa kumshinda Modric kwa mwaka huu, amefanya mambo makubwa sana na ndio maana hata Ulaya amechukua tuzo ya mchezaji bora,” ameongeza.

Kuhusu kuondolewa kwa Lionel Messi kwenye orodha ya mwisho ya wachezaji bora wa FIFA, Rakitic amesema ni jambo la kawaida japo kwake anaamini mchezaji huyo alitakiwa kuendelea kuwa miongoni mwa washindani waliotajwa.

“Wakati mwingine mambo yanakwenda na wakati, japo mashabiki wanaweza kulaumu mengi nikiwepo na mimi, lakini Messi kuondolewa katika orodha ya mwisho ilikua kama bahati mbaya, ninaamini angeweza kushindana na waliopo, na kufikia hatua fulani,” amesema.

Mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa FIFA kwa mwaka 2017/18 anatarajiwa kutangazwa katika hafla itakayofanyika Septemba 29 jijini London, Uingereza.

Tetesi za penzi la Tiwa Savage na Wizkid zamuamsha mumewe wa zamani
LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma Septemba 11, 2018