Agizo limetolewa kusakwa kwa mkandarasi wa mradi wa maji wa Itso uliopo katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma arudi kumalizia mradi huo haraka kabla hajachukuliwa hatua nyingine.

Hayo yamesemwa mapema hii leo na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua mradi huo, Jafo amesema mkandarasi huyo kutoka kampuni ya Audancia anatakiwa kurudi eneo la mradi haraka akamilishe mradi kama mkataba wake unavyoelekeza.

“Mmtake arudi haraka hapa kwenye eneo la mradi au kama ikishindikana achukuliwe hatua za kisheria kwa kukamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani kutokana na kushindwa kutekeleza mkataba,”amesema Jafo.

Aidha, amesema kuwa Mkandarasi huyo ametoweka eneo la mradi huku akiwa amefunga mabomba yenye ubora wa chini kwenye njia kuu ambapo amesema kuwa ni kinyume cha mkataba.

Pia ameagiza mkandarasi mshauri wa mradi huo  O&A  Company LTD kutafutwa kwani ameshindwa kusimamia mradi huo ipasavyo na kuruhusu kazi  hiyo ifanyike kinyume cha mkataba na kuruhusu mkandarasi atoke eneo la mradi wakati vituo vinne havitoi maji kati ya vituo kumi vya mradi.

Hata hivyo, Jafo ametoa onyo kwa wakandarasi washauri na wakandarasi wa ujenzi wa maji ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao kwamba hivi sasa kazi zilizo chini ya Ofisi ya Tamisemi watazisikia kwenye bomba.

 

Video: Makonda aomba Boti kutoka jeshi la China
Samia amuwakilisha JPM mkutano wa wakuu wa nchi SADC