Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amekiri kupokea barua ya chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) inayolamikia mwenendo wa uchaguzi wa uongozi wa serikali za mitaa.

Akizungumzia hali ya zoezi la uchukuaji fomu Jijini Dodoma Oktoba 30, 2019, Jafo amesema tayari wameanza kuzifanyia kazi dosari zilizojitokeza na kuwataka wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia kanuni ili kuondoa kasoro na kuepuka malalamiko yaliyoanza kutolewa.

“Mbali na barua hiyo pia ofisi imepokea malalamiko kutoka kwa vyama vya Siasa, wadau mbalimbali na watu binafsi sasa wasimamizi wa uchaguzi wanatakiwa kuzingatia kanuni ili kuondoa kasoro na kuepusha malalamiko,” ameongeza Jafo.

Amesema kiujumla zoezi hilo limeenda vizuri licha ya kuwa na dosari kwa baadhi ya maeneo ambayo zoezi hilo lilishindwa kufanyika kiufasaha na kusema watahakikisha zinafanyiwa kazi ili uchaguzi uweze kuisha kwa amani na utulivu.

“Tuna kata 3959 na Kati ya kata hizo ni 72 tu ambazo zilikuwa na dosari na zoezi hilo halikufanyika kiufasaha ambapo miongoni mwa maeneo yaliyokuwa na malalamiko ni Liwale Lindi, Moshi, Sengerema na Songwe lakini kiujumla zoezi linaenda vizuri” amefafanua Waziri Jafo.

Aidha katika hatua nyingine Jafo amevitaka vyama vyote vya siasa kuhakikisha vinafuata kanuni, sheria na masharti wakati wote wa zoezi la uchukuaji na Urejeshaji fomu za ugombea wa uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuepusha uvunjifu wa sheria.

Amesema zoezi hilo ni la siku saba hivyo Wizara yake ambayo ndio msimamizi wa uchaguzi huo bado wanaendelea kuzifanyia kazi dosari zote ambazo zimejitokeza na kuwasilishwa kutoka katika maeneo yenye malalamiko.

“Maeneo yote ambayo zoezi hili halikwenda vizuri wawasilishe malalamiko yao kwenye kamati za rufaa na maadili zilizopo katika maeneo yao ili kuondolewa kwa dosari ambazo wanahisi hazikuwekwa vizuri wakati wa zoezi hilo,” amebainisha Jafo.

Kuhusu maagizo aliyoyatoa Waziri jafo amesema hayajapuuzwa isipokuwa changamoto zilizojitokeza ni za kawaida ambazo hutokea katika uchaguzi wowote Duniani na zitaendelea kutatuliwa na ofisi yake kwa weledi.

Oktoba 29, 2019 CHADEMA ilitangaza kuiandikia barua ofisi ya Rais TAMISEMI juu ya uwepo wa dosari kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika nchini kote Novemba 24, 2019 kwa wagombea wake kunyimwa fomu huku maeneo mengine wakipewa fomu zisizosainiwa.

Jurgen Klopp: Sitapeleka timu uwanjani
Abalora wa Azam FC aitwa Black Stars, #BringBackTheLove kuwapeleka AFCON 2021