Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewataka maafisa habari wa vitengo na wizara kuwa wabunifu na kutumia weledi kutoa taarifa kwa umma kuhusu kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Akizungumza leo jijini Arusha katika kikao kazi cha maafisa mawasiliano serikalini, Waziri Jafo amesema kuwa maafisa mawasiliano wengi kwa sasa hawafanyi kazi zao ipasavyo.

Amesema kwakuwa maafisa mawasiliano wengi wanaamini wana uhakika na ajira yao tofauti na waandishi wa habari wa kampuni binafsi za habari, wamekuwa wavivu kutekeleza kwa kasi majukumu yao na kwamba wakati mwingine juhudi zinazofanywa na maafisa kumi wa serikali zinalingana na mwandishi mmoja mahili wa chombo binafsi cha habari.

Aidha, Jafo amesema kuwa baada ya kikao kazi hicho, wizara yake itawaondoa maafisa habari wote ambao wataonekana kushindwa kutekeleza majukumu yao ili wawaajiri watu wengine watakaoweza kufanya kazi hiyo ya kuutarifu umma kuhusu utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

“Maafisa habari wa taasisi zilizo chini ya wizara yangu (TAMISEMI) ambao hawatatosha kutimiza wajibu wao baada ya mafunzo mliyopata, tutawaondoa na kuwapa kazi watu wengine,” alisema Jafo.

Katika hatua nyingine, alizitaka halmashauri na mamlaka za mikoa kuhakikisha zinanunua vifaa vinavyotakiwa ili kuwawezesha maafisa mawasiliano/habari kufanya kazi zao ipasavyo na kuendana na ukuaji wa teknolojia. Amesema anafahamu changamoto nyingi zinazovikabili vitengo vya habari na mawasiliano Serikalini na atahakikisha wizara yake inazitatua.

Amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia, maafisa habari wa Serikali wanapaswa kuhakikisha wanatumia mitandao ya kijamii ipasavyo ili kutowapa nafasi watu wenye nia mbaya wanaoeneza taarifa za uongo zenye lengo la kuchafua taswira ya nchi.

TFF yatoa ofa kwa mashabiki, kesho kuingia bure shamba la bibi
Serikali yamburuza Zuma mahakamani kwa ufisadi