Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo ameagiza ndani ya siku kumi na nne kwa Halmashauri 31 ambazo zilishindwa kuwasilisha fedha zilizotengwa kwa ajiri ya lishe katika halmashauri zao kujieleza kwanini hazikufanya hivyo.

Ametoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua kikao kilichowakutanisha wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, waganga wakuu wa mikoa, wawakilishi toka taasisi ya chakula na wadau wa maendeleo waliokutana kutathmini hali ya lishe hapa Nchini na mahali walipofikia katika mpango wa kwanza wa lishe wa Agosti 2018 hapa Nchini.

Amesema kuna halmashauri 31 hazikutoa fedha zilizotengwa kwa ajiri ya kutekeleza hali ya lishe katika maeneo hayo hali iliyosababisha kushindwa kutekelezwa kwa malengo ya lishe ndani ya halmashauri hizo.

“Ni agize ndani ya siku kumi na nne halmashauri 31 zitoe maelezo ya kina kwa wakuu wao wa mikoa kwanini hazikutoa fedha zilizotengwa ndani ya halmashauri hizo kwa ajiri ya lishe kwanini hazikufika, na ninyi wakuu wa mikoa baada ya siku hizo kumi na nne baada ya hapo nipate maelezo ya kwanini zilishindwa kutekeleza mikataba hiyo wakati halmashauri nyingine zaidi ya mia mija zimetekeleza,”amesema Jafo

Aidha, Jafo amekemea vikali tabia ya wakuu wa idara ambao hawafiki kwenye semina zinazohusu lishe na kuwaagiza watumishi wengine ambao hawana uelewa katika sekta hizo na kusababisha elimu hiyo kutokufikia mahala husika kwa uzembe wa wakuu wa idara hizo.

Pia ameagiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanatoa elimu ya lishe kwa akina mama wajawazito wanapofika kliniki kabla ya kujifungua na watengeneze vipeperushi ambavyo  vitasaidia kupeleka elimu kwa jamii na kuchukua hatua.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika la GAIN linalojihusisha na elimu ya lishe, Archard Ngamela amesema kuwa changamoto kubwa kwenye lishe ni wasindikaji wadogo wadogo hawaweki virutubisho katika bidhaa za vyakula na kusababisha kuenea kwa tatizo la lishe.

CUF yazidi kupukutika, wengine 11 watimkia CCM
Miili ya watu waliouawa New Zealand yaanza kukabidhiwa kwa familia