Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji  Damian Lubuva ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kujifunza uzoefu wa tendaji wa  Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (TKU) ili kuimarisha utawala bora nchini.

Jaji Lubuva ametoa wito huo wakati akieleza uzoefu wake juu ya utendaji kazi wa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (TKU) wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Tume hiyo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Alisema pamoja na TKU kukabiliwa na changamoto nyingi katika inatekeleza majukumu yake wakati huo lakini ilifanya kazi zake kwa ufanisi kutokana na malalamiko ya wananchi yaliyoshughulikiwa kwa wakati huo.

“Katika hali na mazingira ya Tume ya wakati huo, bila kusita nashawishika kusema kuwa Tume ya Kudumu ilianzishwa wakati ambapo si watu wengi kwa bahati mbaya Afrka ambao walijali haki za binadamu na utawala bora” alisema Jaji Mst. Lubuva.

Aliongeza kuwa itakuwa si kusifia kusema kuwa TKU ilifanya kazi nzuri katika kipindi chake cha miaka 32 kwani ulikuwa wakati ambapo Tanzania ndio ilikuwa imejikomboa kutoka utawala wa Kikoloni na ilijitahidi kuendesha shughuli za maendeleo kwa wananchi.

Hata hivyo alisisitiza kuwa walithubutu kwa mwalimu kuleta wazo la kuanzisha TKU ili kunusuru wananchi kutakona na madhila ya matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi na watendaji kwa wakati huo.

“Kwa upande mwingine Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ina kibarua kizito katika kutekeleza majukumu yake katika mazingira ya sasa ambapo tume hii si rahisi kuelezea kwa wananchi kwa nini isifanikiwe zaidi ya TKU”

Alisema THBUB tofauti na TKU ina bahati ya kujifunza kutokana na uzoefu wa tume hiyo ya kudumu katika mazingira ya sasa kulinganisha maendeleo na uelewa wawananchi kiujumla kuhusu haki zao za kimsingi kisiasa na kiutawala.

“Hivyo tunaposherehekea miaka 50 ya Tume ya Uchunguzi ni halali kusema kwamba ilikidhi haja na matakwa ya wananchi kwa wakati huo kuweka misingi imara ambayo THBUB itaitumia katika juhudi za kusonga mbele”alisema Jaji Mst. Lubuva.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment ya Utuishi wa Umma Mhe. Angellah Kairuki alisema lengo kubwa la Serikali kuanzisha TKU ilikuwa ni kumlinda mwananchi na lilifanikiwa kwa kushughulikia malalamiko 39,000 kwa kipindi cha miaka 35.

“Aidha malalamiko yaliyopokelewa katika kipindi cha miaka 15 (2001-2016) ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni 32,000 na hivyo kufanya idadi ya malalamiko ya miaka 50 kufikia 71,000” alisema Mhe. Waziri Kairuki na kuongeza kuwa:

“Idadi hiyo inaonesha jinsi vyombo hivi vilivyo na manufaa kwa wananchi wanyonge.Baadhi ya malalamiko yaliyopokelewa ni kuhusu vitendo vya unyanyasaji, masuala ya utumishi, kuchelewa kutekeleza wajibu, , kukataliwa kuomba rufaa, kutrofuata taratibu za kisheria, mirathi, matumizi mabaya ya mali ya umma na migogoro ya ardhi”

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bahame Nyanduga alisema Maadhimisho ya Miaka 50 ya TKU yamekwenda sanjari na kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuanzisha Tume hiyo ikiwa ni taasisi ya kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma kwa wananchi.

“Pili ni kujikumbusha huko tulikotoka na kujifunza kutokana na kazi za TKU, changamoto na na mafanikio iliyoyapata na mwelekeo unaotakiwa katika kuhakikisha dhana ya uwajibikaji na utawala bora zinaendelezwa nchini Tanzania” alisema Nyanduga.

Katika maadhimisho hayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi walipata Tuzo na Cheti cha kutambua mchango wao kuweka misingi ya uwajibika na utawala Bora

Live: Mapokezi ya Mfalme wa Morocco uwanja wa ndege Dar muda huu
Ziara ya Makamba yabaini uwepo wa Mafuta ya ‘Dizeli’ kwenye visima vya maji