Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amewataka mawakili nchini kujitahidi kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha kwani imekuwa changamoto kwa wasomi wengi wa taaluma hiyo.

Akizungumza jana katika Mahafali ya 59 ya Shule Kuu ya Sheria kwa Vitendo (Law School) jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu alisema kuwa amepata uzoefu wa kuzungumza na wahitimu wote akiwapima uwezo wao wa kisheria pamoja na matumizi ya lugha ya Kiingereza ambayo amesema kuwa haikwepeki katika taaluma hiyo, na kwamba amebaini lugha hiyo inawapa shida wengi wao.

“Binafsi nilipata nafasi adhimu sana kwa mujibu wa kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Mawaliki kukutana ana kwa ana na kila mmoja wenu kinachomtaka Jaji Mkuu ajiridhishe kama wakili mtarajiwa ana sifa stahiki,” alisema Jaji Mkuu.

“Niseme kuwa ufasaha katika kujieleza kwa lugha ya Kiingereza ni changamoto inayotakiwa kufanyiwa kazi, au uongo? Alihoji.

Aliwataka Mawakili hao kuhakikisha wanawekeza katika kujiendeleza ili waifahamu lugha hiyo kwa ufasaha wakitumia pia maendeleo ya Teknolojia ha Habari na Mawasiliano.

Mahafali hayo ambayo yalishuhudia wanasheria 909 wakiapishwa kuwa mawakili, yalihudhuriwa pia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi, Rais wa Chama Cha Wanasheria (TLS), Fatma Karume pamoja na baadhi ya Majaji Wastaafu.

Mawakili hutumia lugha ya Kiingereza zaidi hususan wanapokuwa katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa. Pia, sheria nyingi hasa za kimataifa wanazopaswa kuzifanyia kazi zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 15, 2018
Mo Salah agusa rekodi ya Okocha akibeba tuzo ya Mchezaji Bora Afrika