Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amesimulia mazungumzo kati yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuhusu uteuzi wa majaji wapya.

Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam, katika tukio la kuwaapisha majaji walioteuliwa wiki iliyopita, Jaji Mkuu amesema Rais Magufuli ndiye aliyemkumbusha kuhusu ombi lake la kuongeza idadi ya majaji ili kupunguza mzigo wa kesi mahakama kuu.

“[Mheshimiwa Rais] uliniuliza unataka majaji wangapi, nikakwambia una majina 60 mezani kwako. Nashukuru ulipopata takwimu zetu wewe ulikuwa wa kwanza kunikumbusha hali ya majaji Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani si mzuri,” alisema Jaji Mkuu.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi huo akieleza kuwa hivi sasa kesi zinazosikilizwa na Jaji mmoja katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa zitapungua.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu aliwataka majaji walioapishwa kuzingatia viapo vyao na kujiepusha na mgongano wa maslahi kwa kutumia vyeo vyao kufanikisha biashara zao binafsi.

Aliwaasa pia kutochagua maeneo watakayopelekwa kufanya kazi hiyo kwani itakuwa ni kinyume cha viapo vyao.

Majaji walioapishwa leo, waliteuliwa na Rais Magufuli, Januari 27 mwaka huu.

Tido kurudishwa Mahakamani, Jamhuri wakata rufaa
Bundi atua ndani ya Bunge, Spika Ndugai awatoa hofu wabunge