Jaji Mkuu wa Kenya, David Maranga amesema tangu kutolewa kwa uamuzi wa kubatilisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, mhimili huo umekuwa ukitishiwa.

Kupitia tamko lake kwa umma, Jaji Maranga ameeleza kuwa kumekuwa na vitendo vya kuitishia mahakama kwa kufanya maandamano yanayoambatana na vitendo viovu.

“Maandamano yamejikita katika vitendo viovu na vurugu, vinaonesha wazi kuwa vinalenga kuitishia Mahakama,” alieleza.

Tamko hilo limekuja kufuatia maandamano makubwa yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini humo kupinga uamuzi huo wa Mahakama uliobatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta uliokuwa umetangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya IEBC.

Katika uamuzi wake, Mahakama ilieleza kuwa uchaguzi huo ulikuwa na kasoro nyingi na kwamba haukuwa wa haki.

Kwa mujibu wa uamuzi wa Mahakama uliozingatia Katiba ya nchi hiyo, uchaguzi wa marudio unapaswa kufanywa Oktoba 17 mwaka huu ukisimamiwa na IEBC.

Hata hivyo, upande wa NASA ukiongozwa na Raila Odinga, ambao umeshinda kesi hiyo umeendelea kupinga IEBC kuandaa tena uchaguzi huo wakidai ni wahalifu ambao wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na sio kupewa kazi nyingine.

Trump: Tutaigeuza mavumbi Korea Kaskazini
Majaliwa atoa neno kuhusu watu wasiojulikana