Viongozi wa umma wametakiwa kuwa makini na taarifa zao wanazojaza katika Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa sababu taarifa zao ni nyeti na ujazaji wake ni jambo la Kikatiba.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Maadili Jaji (Mst.) Harold Nsekela kwa nyakati tofauti hivi karibuni alipokutana na viongozi wa mikoa ya Mtwara na Iringa.

Amesema kuwa taarifa za Tamko ni zao binafsi nani nyeti, hivyo wakiwapa watu wasiohusika kumpelekea taarifa hizo harafu baadae zikavuja asilaumiwe.

“Leteni Matamko yenu nyinyi wenyewe msihatarishe siri zenu, nyinyi ni watu wakubwa katika nchi hii, siri zenu zikivuja mtahatarisha heshima ya taifa letu kwasababu mmepewa dhamana kubwa ya kuwaongoza wananchi,” amesema Jaji Nsekela

Aidha, baadhi ya viongozi wa umma wamekuwa na tabia ya kuwatuma watu wasiohusika kupeleka matamko yao katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili kila ifikapo Desemba 31 ya kila mwaka.

Kwa mujibu wa Kamishna Nsekela, kujazia Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kitendo cha kuidharau Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ofisi husika kwa ujumla.

Kamishna Nsekela ameagiza Wakuu wa Kanda wanaosimamia Ofisi za Sekretarieti ya Maadili kuwaita viongozi wote waliojazia matamko yao katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili kuja kwa gharama zao na kuwahoji kuhusu mali zao walizojaza katika matamko yao kwa kulinganisha tamko la mwaka 2018 na matamko ya miaka ya nyuma.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 kifungu cha 9 (1) (a) na (b) kila kiongozi wa Umma anatakiwa kuwasilisha Tamko lake la Rasilimali na Madeni siku 30 baada ya kuteuliwa na kila ifikapo tarehe 31 Desemba ya kila mwaka.

Video: Dawa ya kumdhibiti mwanaume anayechepuka
Tanasha uso kwa uso na mama Dangote, Mashabiki wamtolea povu Diamond