Waziri Mkuu wa zamani, Jaji (mstaafu) Joseph Warioba amesema hali ya kisiasa nchini imekosa itikadi na sera hali iliyosababisha wananchi kushindwa kuelewa wanapelekwa wapi na viongozi ama wanasiasa waliowachagua.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mhadhara wa tatu ulioandaliwa na Kavazi la Mwalimu Nyerere uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, akiwa mgeni rasmi, Jaji Warioba alisema kuwa viongozi wa kisiasa siu hizi hawaendi kwa wananchi kuzungumzia sera na namna ya kutatua matatizo ya wananchi badala yake huenda kwa lengo la kushtakiana na kulalamika kwa wananchi kuhusu matatizo yao binafsi.

“Nilishasema wakati mmoja, huko nyuma viongozi wetu hawa…. akina Kahama (Gerge Kahama, Waziri Serikali ya Awamu ya Kwanza) kazi yao ilikuwa ni kuhangaika na matatizo ya Taifa na matatizo ya wananchi. Siku hizi viongozi wanachukua matatizo yao wanataka wananchi ndio wayashughulikie,” alisema Jaji Warioba. “Yaani wananchi ndio sasa washughulikie matatizo ya viongozi,” aliongeza.

Aidha, Jaji Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema kuwa ingawa Mwalimu Nyerere alipinga kwa nguvu zote uwepo wa ukabila nchini, hivi sasa umeibuka ugonjwa mwingine unaofanana na ukabila kwa kuunda ‘makabila ya vyama vya siasa’ yanayosigana sio kwa sera bali kwa uhasama.

“Siku hizi yameibuka makabila mapya kabisa. Kuna kabila CCM, kabila Chadema, CUF… yamekuwa makabila na yanakuwa na uhasama. Siku hizi hata kwenye misiba wanasiasa wanabaguana,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mzee Warioba alivikosoa vyombo vya habari kwa kujikita katika kuzungumzia siasa na watu badala ya kuripoti kuhusu masuala ya maendeleo.

Aliwataka wanasiasa kuitafsiri demokrasia kwa mtazamo wa kuleta maendeleo na sio kufikiria tu kukamata hatamu za madaraka japokuwa lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola.

Video: Serikali kununua ndege 'keshi' imeepuka kuliwa - Prof. Maghembe
Tukumbushane baadhi ya ahadi za JPM kipindi cha uchaguzi