Siku moja baada ya Mwanasiasa mkongwe, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kuwaomba viongozi wastaafu kumshauri Rais John Magufuli kuikutanisha Serikali na Chadema ili kuvunja UKUTA kwa amani, Jaji Joseph Warioba amejibu.

Jaji Warioba amesema kuwa suala hilo lisichukuliwe kama tatizo la Rais John Magufuli pekee bali ni tatizo la watu wote nchini.

“Ni wajibu wa Watanzania wote kuhakikisha wanalinda hali ya amani nchini badala ya kuliona hilo… kusema jambo hili halimhusu Rais John Magufuli pekee, linamhusu mtu mwingine yeyote. Tumsaidie msajili katika hili, hili sio tatizo la mtu mmoja bali ni la nchi nzima, tusimuachie Rais wetu,” Jaji Warioba amekaririwa.

Amesema kuwa badala ya kumjibu Mzee Kingunge, ni vyema kumpa nafasi Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kuwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa ili kujadili kwa lengo la kutafuta muafaka.

Aidha, Jaji Warioba alisema kuwa wao kama wazee wamekuwa wakimshauri Rais kwa mambo mengi, lakini ushauri huo hawautoi kupitia vyombo vya habari.

“Kweli tuko kimya lakini ukimya huo usitafsiriwe vibaya kuwa hatumshauri Rais Magufuli, sisi kama viongozi wastaafu tunamshhauri rais lakini sio katika vyombo vya habari,” alisema.

Video: Msanii mkali wa Nigeria ‘YCEE’ kuizulu Dar
Audio: Makonda atoa wito kwa Haki za Binaadamu, awataka kulaani mauaji ya Polisi Dar