Suala la mshambuliaji Mbwana Samatta kuwa njiani kutua kwenye klabu ya AS Roma ya Italia, limechukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii tangu asubuhi ya hii leo, na kuzua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Tanzania.

Samatta alisajiliwa na klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji, mwezi Januari mwaka huu na uhamisho wake ulikua wazi na ulimfurahisha kila mpenda soka hapa nchini, lakini suala la kuelekea AS Roma limekua la ghafla na kugubikwa na usiri mkubwa.

Kutokana na hali hiyo, Dar24.com imefanya mazungumzo na meneja wa mshambuliaji huyo ambaye kabla ya kutimkia nchini Ubelgiji alikuwa akicheza soka la kulipwa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwenye klabu ya TP Mazembe ambayo aliisaidia kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2015.

Jamal Kisongo ambaye ni meneja na mlezi wa Samatta, amesema hakuna lolote kuhusiana na hilo na Samatta anaendelea na maandalizi katika kikosi chake cha KRC Genk kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.

“Nimesikia pia, kuna watu kadhaa wameniuliza pia. Lakini ukweli ni hivi… Mbwana anaendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Ubelgiji,” Kasongo ameiambia Dar24.

“Hakuna lolote kuhusiana na Roma hadi sasa labda kama litakuja baadaye. Mawakala wake wote wanalijua hilo. Timu haiwezi ikafanya mawasiliano ya kumuuza bila ya kuwaeleza mawakala wake, meneja wake. Ndiyo maana nasema labda suala hilo lije baadaye,” amesema.

Magufuli amtumbua jipu mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya TIB
Video: Makonda amezitaja adhari za uvutaji Shisha