Kesi inayowakabili viongozi wa zamani wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Jamal Malinzi (Rais) na Katibu wake Selestine Mwesigwa imesogezwa mbele hadi Novemba 30, mwaka huu sababu upelelezi haujakamilka.

Upande wa mashitaka na mawakili wa utetezi katika kesi hiyo inayoendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam umetakiwa kuongeza juhudi katika kufuatilia jalada la kesi hiyo ya utakatishaji fedha, lililopo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilboard Mashauri alitoa maelekezo hayo wakati shauri hilo lilipotajwa na kuibuka kwa hoja ya jalada hilo kuwepo kwa DPP kwa zaidi ya siku 37.

Awali, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Swai alidai jalada la kesi hiyo bado lipo kwa DPP na uongozi wa Takukuru  wanalifuatilia, hivyo aliomba shauri liahirishwe na kupangiwa tarehe nyingine.

Wakili wa utetezi, Abraham Senguji alidai kutokana na mgongano wa ofisi ya DPP na Takukuru, wateja wao ndio wanaumia kwa mashitaka yasiyo na dhamana.

Alidai  kama upande wa Jamhuri hauwezi kukamilisha upelelezi,  waiondoe kesi hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na pale watakapokamilisha upelelezi, wawarejeshe ili iendelee.

Pia aliiomba kama upande wa jamhuri  kama umeshindwa kuendesha kesi hiyo, mahakama iwaachie huru washitakiwa hao.

Akijibu hoja hizo, Wakili Swai alidai  anakubaliana na kifungu hicho cha 91(1) ambacho kinampa DPP mamlaka ya kuifuta kesi wakati wowote pale anapoona inafaa na hata kuirejesha pia.

Swai alidai washitakiwa hao hawatatendewa haki kwa sababu wataachiwa huru na kuwakamata tena na shauri hilo kuanza upya hivyo itakuwa usumbufu kwa washitakiwa.

Alisema Takukuru wakimaliza uchunguzi ni lazima jalada liende kwa DPP alipitie na atoe maelekezo kama upelelezi uliofanywa unajenga kesi ama la.

Alidai makosa ya kughushi yanahitaji utaalamu katika kuyathibitisha na yanachukua muda mrefu katika uchunguzi.

Swai aliomba muda wa kufuatilia jalada hilo. Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hadi  Novemba 30, mwaka huu kwa kutajwa.

Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo  ni  aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Celestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga.

Malinzi na wenzake  wanakabiliwa na mashitaka 28, yakiwamo ya utakatishaji fedha wa Dola za Marekani, 375,418.

Malinzi, pamoja na aliyekuwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29, mwaka huu baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya shirikisho hilo iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.

Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa TFF, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.

Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani, lakini akashindwa kutetea nafasi yake Agosti 12, mwaka huu kutokana na kesi hiyo huku aliyekuwa Makamu wake, Wallace Karia akiwa Rais mpya wa shirikisho.

Video: Nairobi yageuka uwanja wa vita mapokezi ya Odinga
Wapangaji kulipa kodi ya mwezi mmoja