Nahodha Msaidizi na Beki wa zamani wa Liverpool Jamie Carragher, amesema meneja wa Washika Bunduki wa Kaskazini mwa London Mikel Arteta, ana kazi kubwa ya kufanya, ili kukiwezesha kikosi chake kuwa na makali kwa siku za usoni.

Carragher, amesema maneno hayo baada ya kukifuatilia kikosi cha Arsenal, kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Manchester City, ambao waliibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri, juzi Jumatano usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Caragher, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, amesema kikosi cha Arsenal hakiko vizuri na kilionekana dhaifu wakati kikipambana na Manchester City, huku akionya kuwa Arteta anahitaji kufanya kazi kubwa kukibadili kikosi chake.

Mchezo huo ulikuwa wa kwanza kwa Arsenal kwenye Ligi Kuu England iliyosimama kwa miezi miwili kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona, lakini wakaruhusu idadi kubwa ya mabao uwanjani Etihad.

“Sikutarajia kuona kitu tofauti na kile nilichokiona kwenye mchezo ule, kusema la ukweli. Nilichokiona ambacho Arsenal wamekifanya ndio ninachotokea kwa karibu misimu 10 sasa, hakukuwa na tofauti kubwa,” alisema beki huyo aliyeshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Liverpool.

Katika mchezo huo, Arsenal walianza kupotea mapema kabla ya kipindi cha kwanza baada ya beki wake David Luiz kufanya kosa la kizembe na kumpa nafasi Raheem Sterling kupachika bao la kwanza.

Mbrazili huyo aliyeingia kuchukua nafasi ya Pablo Mari aliyeumia mapema tu, alizamisha jahazi la Arsenal kwa mara nyingine baada ya kumfanyia madhambi winga wa Man City, Riyad Mahrez ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru penalti iliyozamishwa wavuni na Kevin De Bruyne.

Mbali na Man City kuzawadiwa penalti, Luiz alilimwa kadi nyekundu na kuifanya Arsenal kucheza ikiwa pungufu na kinda Phil Foden akafunga kufuli kwenye jeneza la Washika Bunduki hao kwa kupiga bao la tatu.

Kutokana na hilo, Caragher alisema kuwa: “Arsenal hawako vizuri. Sioni dalili kama wanaweza kuingia ndani ya Top Four kwani, wana tofauti kubwa ya pointi.”

Elma Aveiro amshambuliaji Sarri
Young Africans waingia kambini Dar