Nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya England, Wayne Rooney, hiii leo hatoanzishwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Hispania.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Roy Hodgson amethibitisha kumuweka pembeni mshambuliaji huyo, kwa lengo la kumpumzisha na kutoa nafasi kwa wachezaji wengine.

Hodgson, amesema tayari ameshazungumza na Rooney juu ya jambo hilo, na wamekubaliana kwa dhati hivyo anatarajia kumtumia mshambuliaji tegemeo wa klabu ya Leicester City, Jamie Vardy, ambaye amemuita kikosini kutokana na umahiri mkubwa anaoendelea kuuonyesha katika ligi ya nchini England.

Amesema maamuzi hayo katu hayawezi kuathiri mfumo atakaoutumia kikosini mwake, kutokana na kuamini kwamba Jamie Vardy, anatosha kuziba pengo la Wayne Rooney ambaye pia ni nahodha wa Man Utd.

Hata hivyo amewahakikishia mashabiki wa soka nchini England na kwingineko duniani kote, kwa kusisitiza kumtumia Rooney katika kikosi chake cha kwanza ambacho kitapambana na timu ya taifa ya Ufaransa kati kati ya juma lijalo.

Kikosi cha England, kinatarajia kuitumia michezo hiyo miwili ya kimataifa ya kirafiki, kwa lengo la kujiweka vyema kabla ya kuelekea nchini Ufaransa mwezi juni mwaka 2016, tayari kwa fainali za mataifa ya barani Ulaya.

Azam FC Yaendelea Kujiimarisha Kibiashara
Marc Wilmots Amuweka Pembeni Vincent Kompany