Wadau wa Elimu Mkoani Kigoma wameombwa kuunga mkono jitihada za serikali za kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu ili kuleta uwiano sawa wa ufaulu na wavulana suala linalosemekana kusaidia kukomesha vitendo vya watoto kupata mimba wakiwa shuleni.

Hayo yamesemwa na Afisa Elimu wa Mkoa huo, Juma Kaponda alipokuwa akizungumza na walimu wa Kata ya Kibondo Mjini katika hafla ya kupongezana baada ya kufanya vizuri upande wa elimu.

Amesema kuwa mkoa wa Kigoma unakumbwa na janga kubwa la mimba mashuleni kwa watoto wa kike ambapo kwa mwaka 2017/2018 jumla ya wanafunzi wa kike 190 wamepata mimba ambapo wanafunzi 85 ni wa shule za msingi na wanafunzi 105 wakiwa ni wanafunzi wa shule za sekondari.

Aidha, amesema kuwa wadau wa elimu pamoja na wazazi/walezi wanayo dhamana kubwa ya kushirikiana na serikali kuhakikisha elimu inatolewa kwa mtoto wa kike ili kumuokoa na janga hilo la mimba za utotoni kwa sababu linakatisha ndoto zao.

“Kutokana na ufaulu hafifu wa wanafunzi wetu wa kike tumeanzisha mkakati wa wanafunzi hao kuwa na masomo ya ziada, laini suala la kusikitisha watoto wanaorejea ni wachache suala linalokatisha tamaa, niwaombe wazazi wasiwapangie watoto hao kazi nyingine wawaachie waje shuleni ili waweze kupata elimu,” amesema Mwalimu Kaponda.

Baadhi ya wadau waliokuwepo katika hafla hiyo wametoa maoni yao kuhusu suala zima la elimu katika wilaya nzima ya Kibondo pamoja na mkoa wa kigoma kwa ujumla huku wakiiomba serikali kushirikiana na wadau wengine wa elimu ili kuboresha elimu ya motto wa Kigoma kuwatengenezea mazingira rafiki ya kusomea na kuzipa nafasi na kuzitambua shule binafsi kwa mchango wao.

Mkoa wa Kigoma licha ya kukabiliwa na changamoto ya mimba mashuleni bado unakabiliwa pia na changamoto kubwa ya uhaba wa miundombinu ya madarasa suala lililopelekea zaidi ya watoto elfu 10 kutokuanza masomo yao ya kidato cha kwanza  January 07 mwaka huu shule zilipofunguliwa licha ya kuwa walifahulu elimu ya msingi.

Video: Wakali wa kolabo WCB, wavunja rekodi nyingine na 'Tetema', Tazama
Ulaya, Amerika ya Kusini kuijadili Venezuela