Balozi wa Japani nchini, Masaharu Yoshinda amesema kwamba Serikali yake ipo tayari kukarabati shule zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.

Balozi Yoshinda ameyasema hayo leo Septemba 19, 2016 wakati alipokutana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake Magogoni Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya maafa yalitokea Kagera, ambapo ameomba pia kupatiwa orodha ya mahitaji ya dharura yakiwemo mahema, mablanketi, dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.

Waziri Mkuu, Majaliwa ameishukuru Serikali ya Japani kwa hatua hiyo na kukiagiza Kitengo cha Maafa kilicho chini ya Ofisi yake kuwasiliana na Ubalozi wa Japan nchini na kuwasilisha orodha ya shule zilizoharibika pamoja na mahitaji ya dharura.

Waziri Mkuu pia amepokea msaada wa tani 2.5 za mchele, magodoro 200, mablanketi 100 na fedha taslimu sh. milioni 10 kutoka kwa wadau mbalimbali akiwemo Ofisa Utumishi wa Kampuni ya Chang Qing Inernational Investiment Limited ya nchini, Bi. Anna Jiang aliyetoa magodoro 200 yenye thamani ya sh. milioni sita ili kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko hilo.

Waliotoa misaada wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa Benki ya Exim, George Shumbusho aliyetooa sh. milioni 10 pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Urafiki kati ya Serikali ya Tanzania na China, Bw. Joseph Kahama aliyetoa mchele tani 2.5 pamoja na mabllanketi 100 vyote vikiwa na thamani y ash. milioni 10.

Majaliwa amewashukuru kwa misaada hiyo na kuwaomba wananchi wengine wajitokeze kwa wingi ili kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo ambalo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.

Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 wametibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.

Kufuatia tetemeko hilo pia nyumba  2,063 zilianguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakiiitaji misaada mbalimbali.

Video: Jaji Chande auzungumzia Mpango Mkakati wa Mahakama Tanzania
Majaliwa akutana na Balozi wa Japan nchini