Zaidi ya waokoaji 110,000 wamepewa kazi ya kuwatafuta na kuwaokoa watu walioathiriwa na kimbunga ‘Hagibis’ kilichoikumba Japan, Jumamosi, Oktoba 12, 2019.

Kimbunga hicho ambacho ni kibaya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi kimesababisha vifo vya watu 31 na watu wengine 15 wakiwa hawajulikani walipo.

Janga hilo lilisababisha kuahirishwa kwa mechi tatu za Mashindano ya Dunia ya Rugby ingawa mchezo muhimu zaidi wa kati ya Japan na Scotland uliendelea.

Katika mchezo huo, Timu ya Japan iliwafuta machozi wananchi wake baada ya kushinda 28-21 na kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza.

Kocha wa timu hiyo, Jamie Joseph alitoa heshima zake kwa waathirika wa kimbunga akieleza kuwa ushindi huo uliopatikana ni maalum kwa ajili yao.

“Kila aliyeathiriwa na kimbunga hiki, huu mchezo ulikuwa kwa ajili yenu na ushindi huu ni ajili yenu pia,”alisema kocha Joseph. “Umati wa watazamaji ulikuwa mkubwa kwetu, na leo ilikuwa ziaidi ya mchezo wa kawaida kwetu,”aliongeza.

Ingawa kimbunga hicho kilidhoofishwa na kwenda mbali na ardhi kiliacha madhara makubwa ya uharibifu wa mali na vifo vya watu.

Maelfu ya maafisa wa polisi, vikosi vya moto na majeshi mengine wanaendelea na kazi ya kuwatafuta watu walionasa kwenye maporomoko na mafuriko.

Ni Kenya tena: Mwanariadha wa kike avunja rekodi ya dunia
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 14, 2019