Nyota wa muziki wa bongo fleva, Jay Melody kwa mara ya kwanza ameweka wazi kusitisha kujihusisha na kuwaandikia mashairi ya muziki wasanii wengine kwa kile alichodai kuwa kwa sasa, hayuko radhi kushiriki katika kuwasindikiza wasanii wengine kwenye utajiri.

Jay Melody, ambaye anafanya vizuri na wimbo wake mpya ‘Nakupenda’ ameonyesha kujutia kipindi kigumu alichopitia wakati wa kuwatungia mashairi ya muziki wasanii wengine, akidai hakunufaika kwa kiwango anachostahili kama mtunzi.

Amesema, msanii anayekuwa ameandikiwa nyimbo kupata mafanikio makubwa, ikiwamo fursa mbali mbali zitokanazo na ukubwa wa nyimbo anazokuwa ametungiwa lakini yeye kama mtungaji anakuwa haambulii kitu.

“Kwa sasa nimeacha kuwaandiki watu wasanii wengine, kwa sababu nafocus na mziki wangu na amini nikijitengenezea mimi mwenyewe ngoma itakuwa bora zaidi kuliko nikiwatengenezea watu wengine,” amesema Jay Melody.

Ameongeza kuwa, “Hatutakiwi kuwasindikiza watu kwenye utajiri, tunatakiwa kutengeneza maisha yetu tuwe matajiri sisi wenyewe, so kwa sasa nimeacha na nililiweka wazi hili mapema sana, kwamba sitaweza kumuandikia mtu mwingine tena wimbo kwa sababu hakuna hiyo nafasi.”

Kauli ya nyota huyo, inakuja wakati ambao tayari kumekuwepo na mijadala mbali mbali kuhusu mfumo wa mgawanyiko wa faida itokanayo na kazi ya sanaa ya muziki, wenye kuhusisha watunzi ambao mara zote wamekuwa wakitajwa kama miongoni mwa watu wasionufaika na kazi zao.

Vanessa Mdee 'aamsha popo' za Mziiki hadharani
Waziri Mkuu ahudhuria Mkutano TICAD