Wakongwe wa muziki wa kizazi kipya, Juma ‘Jay Moe’ Mchopanga na Hamad ‘Madee’ Ally wametoa mtazamo wao kuhusu sababu za nyimbo zinazotoka hivi sasa kutokuwa na maisha marefu tofauti na ilivyokuwa kwa nyimbo za zamani.

Wakiongea na The Playlist ya 100.5 Times FM, kwa upande wa Jay Mo amefunguka kuwa nyimbo nyingi za sasa zinakuja na kupotea kutokana nawasanii wengi kuangalia soko na sio ubora wa muziki wanaofanya.

“Vijana wa sasa wakitaka kutoa wimbo utakaoishi miaka 40, basi wafanye wakiwa hawawazi biashara. Kipindi kile tulikuwa hatufanyi wimbo upigwe tu redioni au tupate fame (umaarufu), tulifanya kwa mapenzi yetu na muziki na kuzingatia ubora,’’amefunguka Jay Moe.

‘Kulikuwa na studio kama Bongo Record tunarekodi bure lakini sasa muziki una gharama nyingi kwahiyo wasanii wanafanya muziki biashara la sivyo watapata hasara,’’ ameongeza Jay Moe.

Naye Madee, amesema kinacho fanya nyimbo nyingi hivi sasa kutoishi kwa muda mrefu ni kutokana na ongezeko la wasanii na nyimbo kutoka kwa wingi tofauti na zamani.

Madee

“Sasa hivi wasanii wanatoa nyimbo kila siku. Nyimbo zimekuwa nyingi kwahiyo ni rahisi ngoma zingine kusahaulika, zamani ilikuwa tofauti,” amesema Madee.

Madee ameongeza kuwa wasaniii wa zamani walikuwa wakitumia muda mrefu kutayarisha wimbo kabla kuamua kuutoa na kwamba hiyo ndiyo sababu nyimbo nyingi zilikuwa na ubora na kuishi maisha marefu zaidi.

Kizimbani kwa kula nyama za binadamu
Tanesco kuwashughulikia wafanyakazi wahujumu