Jana ilikuwa siku ya Alhamisi ya kumbukizi ambayo iliambatana na wiki kama mbili za ukimya wa Makala za kumbukizi tukoka Dar24. Lakini kutokana na maombi maalum ya wasomaji, imebidi tufanye kila liwezekanalo kuirejesha siku ya jana kwenye ukurasa huu wa kumbukizi.

Wakati huu, tutavuka mipaka na kulitembelea eneo la Bedford-Stuyvesant, Brooklyn nchini Marekani tukikumbuka tukio la mwaka 1981 la familia ya Mzee Adnis Reeves ambaye hata hivyo alikuwa ameikimbia familia yake kutokana na ugumu wa maisha.

Katika familia hiyo, alizaliwa rapa Sean Carter aka Jay Z ambaye hivi sasa ana utajiri wa $900 milioni, kwa mujibu wa jarida la Forbes. Angekuwa Mtanzania angekuwa nyuma kidogo ya Mohammed Dewji mwenye ukwasi wa $1.9 bilioni.

Mzee Reeves alimuachia mkewe Gloria Carter watoto wanne ambao ni Jay Z na ndugu zake watatu walioishi kwa kubangaiza kwenye mitaa hatari ambayo kila siku milio ya risasi ilikuwa ikisikika. Katika mitaa hiyo biashara ya dawa ya kulevya ilikuwa imeshamiri kwa vijana na bunduki zilikuwa zinamilikiwa kama simu za mkononi za wakati huu na watu walikuwa wakipigana risasi kiholela.

Mwaka 2010, kwa mara ya kwanza, Jay Z alifunguka kwenye mahojiano maalum na Jarida la ‘Weekend’ jinsi ambavyo akiwa na umri wa miaka 12 tu alimpiga risasi kaka yake aliyekuwa teja wa madawa ya kulevya, ambaye alimuibia kidani cha dhahabu alichokuwa ametunza kama sehemu ya kibubu chake.

Jay Z ambaye hivi sasa ni baba wa watoto watatu akijaliwa kuwa na ubavu wake wenye utajiri mkubwa pia, Beyonce Gloria Carter, alieleza kuwa alifungua kibubu chake na akagundua hazina yake imechukuliwa na mtuhumiwa wa kwanza alikuwa kaka yake ambaye alienda kuuza ili anunue madawa ya kulevya.

Anasema hasira zilimzidi umri, akiwa mtoto alichukua bunduki na kufyatua risasi iliyompata kaka yake begani.

“Nilidhani yamekwisha. Nilidhani nitaozea jela,” alifunguka. “Ilikuwa mbaya sana, niliogopa sana, nilikuwa mtoto,” aliongeza.

“Bunduki zilikuwa zimezagaa kwenye mitaa yetu. Haukuwa na haja ya kwenda mbali kupata bunduki. Kulikuwa na matukio ya watu kufyatua risasi mara nyingi, lakini sikuwahi kumpiga risasi mtu yeyote, nilimpiga ndugu yangu,” alisimulia.

Tukio hilo lilimtesa sana Jay Z kiasi cha kuliweka pia kwenye nyimbo zake kadhaa. Kwenye wimbo wake ‘You Must Love Me’, Jigga anarap, “Saw the devil in your eyes, high off more than weed, confused, I just closed my young eyes and squeezed.”

Hata hivyo, kaka yake huyo aliyekuwa anajiuguza na ulaibu wa madawa ya kulevya hakufungua mashtaka dhidi ya mdogo wake. Alipokuwa amelazwa hospitalini alimuomba radhi mdogo wake ambaye alimtembelea na wote walikubaliana kusameheana.

Alipoanza shule alijikuta akisoma kwenye shule ambazo zilikuwa na wanafunzi wengi wenye mizuka ya muziki wa kufokafoka, na yeye ndiko alikokuzia kipaji chake. Aliwahi kusoma shule moja na rapa AZ, na akiwa katika shule ya George Westinghouse Career and Technical Education High School alisoma na rapa Notorious B.I.G pamoja na Busta Rhymes. Hata hivyo, hakumaliza kikamilifu masomo yake.

Kwa mujibu wa Jay Z, katika kipindi hicho alikuwa anauza dawa za kulevya aina ya cocaine na aliwahi kupigwa risasi mara tatu kwenye biashara hiyo haramu.

Hakuiacha ndoto yake na kipaji chake kilizidi kukorezwa na mashindano yasiyo rasimi ya michano katika shule alizokuwa anasoma. Madaftari yake yalijaa mistari ya rap. Mama yake Gloria alikuwa mkali, alianza kukagua daftari ili asione mistari badala yake aone masomo. Ndipo jigga alipoanza kuandika mistari yake kwa kuikariri moja kwa moja kichwani, hali iliyomtengenezea kipaji cha aina yake na kwa miaka takribani 10 alirekodi albam zake bila kuandika kwenye karatasi hata mstari mmoja.

Mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990 alianza kusikika kwenye nyimbo kama ‘The Originators’ na ‘Hawaiian Sophie’. Alipata jina kubwa aliposhindana mara kadhaa na rapa LL Cool J kwenye mashindano ya mtaani ya michano (street hip-hop battles).

Baada ya kukosa kampuni ya kumsaini, Jay Z alianza kuuza CD mtaani mkono kwa mkono. Na mwaka 1995 akiwa na rafiki zake Damon Dash na Kareem Biggs, walikusanya mitaji na kuanzisha Roc-A-Fella Records. Kupitia lebo hiyo, mwaka 1996 Jay Z aliachia albam yake ya kwanza ‘Reasonable Doubt’.

Kuanzia hapo maisha yalibadilika. Yule mtoto aliyeishi uswahili akipishana na risasi kila siku alikuwa rafiki mkubwa wa Rais wa Marekani, Barack Obama katika utawala uliopita, alitembelea Ikulu na kusaidia kwa kiasi kikubwa ushindi wa rais huyo.

Mauzo ya albam zake pamoja na biashara nyingine yalikuwa makubwa kuwahi kuyaota. Mwenyewe anasema, “mimi sio mfanyabiashara, mimi ni biashara.”

Leo, Jigga ni habari nyingine, akiwa anajutia vikali tukio la kumshambulia kaka yake kwa risasi, anasema “nobody wins when the family feuds – hakuna anayeshinda wanafamilia wanapogombana.”

Video: Undani tuhuma nzito za Masele, Mbuge amgomea Spika Ndugai
LIVE: YANAYOJIRI BUNGENI DODOMA LEO MEI 17, 2019