Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke amesema moja ya sababu yake kubwa iliyomsukuma kukubali kutua Simba SC, ni kufanya makubwa na kuifikisha mbali klabu hiyo Kimataifa.

Baleke alisajiliwa Simba SC wakati wa Dirisha Dogo la Usajili akitokea TP Mazembe, ambayo ilimtoa kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu kwenye klabu ya Nejmeh SC ya Lebanon.

Mshambuliaji huyo amesema mbali na kuanza vizuri katika Ligi Kuu akifunga bao moja dhidi ya Dodoma Jiji FC, bado ana malengo mengine ya kufanikisha dhamira ya Simba SC kufika Hatua ya Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Amesema anafahamu ukubwa wa Simba SC katika Michuano ya Kimataifa, hivyo anatamani kuwa sehemu ya wachezaji watakaoiwezesha kufanya vizuri msimu huu, na kuendelea kuwa gumzo nje ya Tanzania.

“Unajua Simba SC ukiwa huko nje inafahamika kutokana na uwezo wake wa kufanya vizuri katika michuano ya Kimataifa, ndicho ninachoona kinakwenda kutokea, lazima tufike mbali na tutapambania hilo.”

“Binafsi nataka niwaambie mashabiki tu kwamba wao wajibu wao ni kuja uwanjani kuishangilia timu yao, sisi kama wachezaji tutapambana kwa ajili yao na Simba yao.”

“Ninaamini tutafanya vizuri kama kawaida ya Klabu hii, ambayo imeendelea kudhihirisha hilo kila inapoingia Hatua ya Makundi Barani Afrika.” amesema Baleke

Simba SC itaanza kupambana dhidi ya Horoya AC katika mchezo wa Kundi B, lenye timu nyingine za Raja Casablanca (Morocco) na Vipers SC (Uganda).

Simba SC itacheza dhidi ya Horoya AC mjini Conakry, katika Uwanja wa General Lansana Conté, Febriari 11 majira ya saa kumi jioni kwa saa za Guinea, huku Raja Casablanca (Morocco) ikiikaribisha Vipers SC (Uganda) Stade Mohammed V, mjini Casablanca, saa mbili usiku kwa saa za Morocco.

KMC FC yaifuata Ruvu Shooting Morogoro
Ruto Vs Kenyatta: IGP aeleza sababu za kumpunguzia Uhuru Kenyatta walinzi