Mkoa wa Kilimanjaro nimewahi kusoma katika kipindi fulani mara baada ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo, chini ya Waziri Mkuu Samwel Marcela kuifunga shule ya Sekondari ya Tambaza na kuwahamisha wanafunzi wa Tambaza kwa kuwatawanya nchi nzima, kuondoa kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule hii ya umma ambayo hadi sasa haina kidato cha Kwanza hadi cha nne kutokana na maamuzi hayo.

Maamuzi hayo ya Serikali yaliyofanyika mwaka 1994 yanisaidia na mimi kuweza kuufahamu kidogo mkoa wa Kilimanjaro, hususani wilaya ya Same, kwani nilihamishiwa shule ya sekondari ya Same.

Unapokuwa mwanafunzi shuleni ni vigumu mno kupata nafasi ya kuelewa mambo ya jamii, hata kama uwe ni mjanja wa namna gani, kwa kuwa jukumu lako la msingi kama mwanafunzi ni kusoma, waswahili wanasema mshika mawili moja linamponyoka.

Nikiwa Same wakati huo niliwafahamu wanasiasa wachache wa eneo hilo kama Chediel Mgonja ambaye alikuwa ni mbunge wa zamani wa Same na miongoni mwa mawaziri wa kwanza kwanza wa wakati wa mwalimu Nyerere. Lakini pia nilimfahamu Baba Askofu Josaphat Louis Lebulu ambaye wakati huo alikuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Same kabla ya kuhamishiwa Jimbo la Arusha.

Habari za wilaya zingine za mkoa Kilimanjaro nilizipata katika simulizi tu za wanafunzi niliyokuwa nasoma nao, wazaliwa wa wilaya hizo wakiwamo Wachaga, Wapare na Wamasai. Japokuwa nilikuwa nikipita tu kama njia kuelekea maeneo mengine lakini siyo kukaa kwa zaidi ya juma moja.

Kwa kuwa sasa nimejaliwa kukaa kwa juma moja nimejaribu kuyaishi maisha ya Wachaga na wale wageni wanaohudumu katika mkoa huu, iwe watumishi wa umma au wale wanaofanya shughuli zao binafsi.
Mtu wa kwanza kumtembea na kuona naye nyumbani kwake ambaye aliweza kunikaribisha kwa mikono miwili bila waa ni Mangi Mkuu wa Wachaga Frank Mareale ambaye alikuwa mwema mno kwangu na nilipata nafasi ya kuzungumza naye mambo kadhaa ya nduguze wachaga mila na utamaduni wao.

Nikiwa na Chifu Mareale mara baada ya kuzungumza naye kwa kuwa na yeye alikuwa akiondoka alinipakiza katika gari yake aina Jeep na kuniacha katikati ya Mji wa Moshi na mie kuendelea na kazi zangu za hapa na pale.

Mwanakwetu mwezenu nimepanda Jeep ya Chifu Mareale.

Waswahili husema kuwa ili kuweza kuifahamu mbuga yoyote sharti la msingi ni kuitembelea mbuga hiyo, mwanakwetu kumbuka kuwa mbugani kuna mengi, unaweza kukutana na mbigili zikakuchoma, lakini nia yako ya kuitembelea mbuga lazima ikamilike ili upate ya kusimulia.

Nikiwa Moshi Mjini niliumwa sikio juu ya dawa ya asili ya Wachaga inayofahamika kama Ngesi ambayo hutumiwa kama tiba kwa kipindi kirefu. Mmea wa ngesi huwa unatoa matunda ambayo hutafunwa lakini pia magome ya mti wa ngesi hubanduliwa na kutumika kama dawa inayoweza kutibu magonjwa mengi kama ilivyo kwa mimea inayatumiwa katika maeneo mengine ya Tanzania kama Mwarubaini.

“Magome ya mti wa ngesi yakichemshwa pamoja na kunywewa yalikuwa kama kinga ya Wachaga wasipatwe na magonjwa mbalimbali. Kwa asili sisi Wachaga ilikuwa ni kawaida watoto wapewe ngesi mara moja au mara mbili kwa mwezi kama kinga ya magonjwa mbalimbali.” Aliniambia Mama Julieti Mosha.

Ili kupata uhakika wa jambo hilo nilimtafuta Dkt Emmanuel Temu ambaye ni Mkurugenzi wa wa Maendeleo ya Utamaduni nchini ambaye amefanya tafiti nyingi juu ya kabila la Wachaga huku nayeye akiyaishi maisha hayo kama Mchaga kwa kuzaliwa.

“Wachaga ni jamii ambayo inajihusisha na ufugaji, kwa kuwa ni wafugaji pia ni walaji wazuri wa nyama. Kabla ya kula nyama tuna utaratibu wa walaji hao kunywa dawa ya ngesi kama kusafisha matumbo yao ili tumbo kuweza kupokea chakula kilichoandalia, ukiondoa kutibu magonjwa.” Alisisitiza Dkt Temu
Matumzi ya NGESI yalianza muda mrefu kwa Wachaga hata kabla ya Wageni kuingia nchi petu. Hii ni dawa ya asili ya Wachaga tangu enzi.

Binafsi kwa kuwa nipo Moshi nitajitahidi kabla ya kufungasha virago vyangu na kurudi Dodoma, ninywe dawa na ngesi angalau na mie nisafishe tumbo na nikifika Chalinze Nyama Dodoma nizifakamie nyama.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Tuzo za Grammy zarejea
Kibaha-Segera kupeta na njia nne