Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema tatizo la saratani kwa Watanzania linaweza kupungua ama kuondokana nalo endapo kutakuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa jengo na mashine mpya za tiba ya mionzi LINAC ambazo ni za kisasa kabisa na kwa Afrika, ambapo Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuwa nazo.

“Tunaweza kujikinga kwa kufuata kanuni za afya zinavyotuelekeza kula chakula bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kuepuka kunywa pombe kupita kiasi na kuepuka matumizi ya tumbaku”amesema Samia Suluhu Hassan.

Mradi wa ununuzi na ufungaji wa mashine mpya za kisasa za tiba ya mionzi umegharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo shilingi bilioni 9.5 zimetumika.

Aidha, Makamu wa Rais amewataka wananchi wote hasa wanawake kufika katika vituo ili kufanyiwa uchunguzi kwani zikigundulika dalili za awali mgonjwa atatibiwa na kupona, huku akiwasisitiza wanaume waanze kuchukua mwamko wa kupima afya zao hasa kupima saratani ya tezi dume.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa katika kipindi kifupi cha miaka mitatu sekta ya Afya imepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo chanjo kwa watoto zimefikia asilimia 98%, upatikanaji wa dawa muhimu ni asilimia 95%, vifaa na vifaa tiba, huduma za mama na mtoto ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.

 

Bosi wa Takukuru afikishwa kortini
Video: Filamu ya "US" ya Lupita Nyong'o yaweka rekodi

Comments

comments