Beki wa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich Jerome Boateng, huenda akawa nje ya uwanja katika kipindi cha msimu wa 2017/18 kilichosalia, kufuatia majeraha aliyoyapata usiku wa kuamkia leo, wakati wa mchezo wa mkondo wa kwanza nusu fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid.

Majibu wa vipimo alivyofanyiwa Boateng, yameonyesha anasumbuliwa na majeraha ya misuli ya paja ambayo huenda yakamchukua majuma kadhaa ili aweze kuwa fit na kucheza tena soka.

“Boateng amebainika kuwa na matatizo ya misuli ya paja lake la mguu wa kushoto, na huenda akakosa sehemu ya msimu iliyosalia,” Imeeleza taarifa iliyotolewa na FC Bayern muda mchache uliopita.

Hata hivyo beki huyo mwenye umri wa miaka 29, ana uhakika wa kucheza fainali za kombe la dunia zitakazoanza Juni 14 nchini Urusi, endapo ataitwa kwenye kikosi cha Ujerumani, ambacho kitaanikwa hadharani Mei 19.

Katika hatua nyingine mshambuliaji wa pembeni wa FC Bayern Munich Arjen Robben, ambaye alilazimika kutolewa dakika za mwanzo za mchezo wa jana dhidi ya Real Madrid, naye anasumbuliwa na misuli ya paja.

Wakati huo huo kiungo Javi Martinez, ambaye alitolewa katika mchezo huo baada ya kuumia kichwa, atakosa mazoezi ya siku kadhaa, lakini ana matarajio makubwa ya kuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kuelekea mjini Madrid juma lijalo.

Madagascar yaanza mazungumzo kumaliza mgogoro wa kisiasa
Klabu ya Fulham kuumiliki uwanja wa Wembley